Mke azima polo kuoa wa pembeni

Na JOHN MUSYOKI

KIVAA, MASINGA

UGOMVI ulizuka katika boma moja hapa, jamaa alipokabiliwa na mke wake wa kwanza kwa kutaka kuuza ploti ili apate pesa za kumlipia mke wa pili mahari.

Duru zinasema, polo alilazimika kuoa mpango wa kando baada ya kumpachika mimba na wakwe wakamsukuma alipe mahari.

Kwa kuwa hakuwa na pesa, aliamua kuuza ploti yake, hatua ambayo haikumfurahisha mke wa kwanza.

Inasemekana mke wa kwanza alipinga hatua ya mumewe ya kuuza ploti ambayo alichangia kununua.

“Una akili timamu wewe? Kama una mpango wa kuuza ploti hii tuliyoinunua mimi na wewe ili umlipie mke wako wa pili mahari sahau. Hautauza ploti hii upende usipende,” mke alimwambia mumewe.

Jamaa alizusha akidai ploti hiyo ilikuwa mali yake.

“Ninauza ploti yangu sio yako. Haufai kulalamika kwa kuwa tayari nilikulipia mahari na wewe pia ni mali yangu,” jamaa alimjibu mkewe.

Hata hivyo, mkewe aliwaka kwa hasira akimlaumu jamaa kwa kupenda wanawake.

“Ulikosa nini kutoka kwangu mpaka ukaamua kuoa mke wa pili? Tamaa ya wanawake utaiacha. Ulijifanya simba ulipomleta mwanamke huyu hapa nikiwa nimenyamaza. Leo hii ni mimi simba hapa na hautaiuza ploti hii. Beba msalaba wako na ukishindwa umrudishe binti ya wenyewe kwao akaolewe na mwanaume mwingine, hata wewe umezeeka sana na hauna adabu kuoa mwanamke wa rika la binti yako,” mke aliwaka.

Polo aliposhindwa kumtuliza mkewe, aliamua kwenda mafichoni kuwaepuka wakwe waliokuwa wakimshinikiza alipe magari. Hakuna anayejua aliko jamaa huyo japo inasemekana huwa anawasiliana na mkewe wa pili ambaye amekuwa akiwatuliza wazazi wake.