• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
DIMBA MASHINANI: Handiboli ya ufukweni yafaidi vijana Pwani

DIMBA MASHINANI: Handiboli ya ufukweni yafaidi vijana Pwani

Na CHARLES ONGADI

MCHEZO wa mpira wa mkono wa ufukweni maarufu kama Beach Handball unazidi kupata umaarufu miongoni mwa vijana jimbo la Pwani.

Handiboli ya Ufukweni inachezwa na wachezaji wanne kila upande tofauti na handiboli ya kawaida inayochezwa na wachezaji saba kila upande. Wachezaji hucheza miguu chuma bila kuvalia viatu ila wanaruhusiwa kuvaa soksi pekee miguuni mwao.

Muda wa mchezo huwa ni dakika 20 tofauti na handiboli ya kawaida inayochukua takribani dakika sitini kukamilika.

Ni mchezo unaoburudisha kutokana na kwamba kuna mabao yanayofungwa kiufundi na kwa madaha yanayopatiwa alama mbili na tofauti na ufungaji wa kawaida iliyo na alama moja pekee.

Vijana wengi Pwani wameweza kugeukia mchezo huu na mwishowe kuangukia ufadhili wa kimasomo unaotolewa na shule za upili na vyuo vikuu mbali mbali nchini.

Kulingana na katibu wa Shirikisho la Handiboli nchini tawi la Pwani Anthony Were, zaidi ya vijana 30 wamebahatika kupata ufadhili wa masomo kupitia mchezo huu.

Stella Clay Awuor,23, mwanafunzi wa zamani wa shule ya upili ya Sega Girls aliangukia ufadhili wa kimasomo katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kupitia ubora wake katika mchezo huu.

Awuor ambaye ni yatima, anaiambia Dimba kwamba alianza kucheza handiboli ya kawaida akiwa na miaka 7 pekee akiwa mwanafunzi.

Awuor aliamua kuacha mchezo wa kuruka umbali (long Jump) akiwa shule ya msingi ya Bar Sauri, Gem kaunti ya Siaya baada ya rai ya mwalimu wake wa michezo.

Aidha, mara baada ya kufaulu katika mtihani wa kidato cha nne kwa kuibuka na gredi ya B hakuwa na matumaini ya kujiunga na Chuo Kikuu kutoakana na hali ya uchochole.

Mwaka wa 2016 aliamua kuyoyomea Mombasa kusaka maisha ila tu kukutana na kocha maarufu wa handiboli nchini Luke Ogot aliyemshauri kujiunga na timu Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) kupalilia zaidi kipaji chake

Baada ya kipindi kifupi tu akaitwa kwa mara ya kwanza katika timu ya taifa mwaka huo huo wa 2016 na kujumuishwa katika timu hiyo iliyoelekea nchini Cape Verde mwaka wa 2019 lakini hakuweza kusafiri kutokana na kubanwa na shughuli za kibinafsi.

Hata hivyo, aliweza kuendelea kuonesha ubora wake katika mashindano ya Vyuo Vikuu akiwakilisha TUM na kuvutia usimamizi wa Chuo kikuu cha Jomo Kenyatta ulioamua kumsajili katika timu yao na kumpatia ufadhili wa kimasomo mwaka wa 2018 anakosomea shahada ya biashara.

Naye Derick Otieno ,27, aliamua kuacha soka na kujiunga na handiboli mwaka wa 2010 baada ya kuvutiwa na mchezo huu akiwa shule ya upili ya Changamwe.

Mwaka wa 2013, Otieno akajipata katika kikosi cha Shule ya Changamwe kilichozuru Unguja kwa mashindano ya kimataifa walikomaliza katika nafasi ya tatu

Mwaka wa 2014 aliitwa katika timu ya taifa ya U18 na kushiriki katika mashindano ya Africa Junior Championship jijini Nairobi.

Hata hivyo, kulingana na Luke Ogot ambaye ni kati ya viongozi wa mchezo huu Pwani ukosefu wa vifaa vya kutosha vya mazoezi ni kati ya changamoto zinazowakabili beach handboli kwa sasa.

You can share this post!

MBWEMBWE: Fernandinho na mkewe ni wapenzi wa michuma ya bei...

Ruth kidedea akiweka rekodi mpya ya dunia mbio za 21km