• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Aliyenaswa kwa video akimtesa mshukiwa wa wizi Ajab Mills atiwa mbaroni

Aliyenaswa kwa video akimtesa mshukiwa wa wizi Ajab Mills atiwa mbaroni

Na WACHIRA MWANGI

POLISI katika Kaunti ya Mombasa wamemtia mbaroni mshukiwa aliyenaswa kwa video akimtesa mwanamume aliyeshukiwa kuiba kutoka kwa Ajab Mills huko Shimanzi.

Mshukiwa, Swabir Mohamed, 33, ambaye pia ni Msimamizi wa Usalama katika kiwanda cha Ajab Mills, Jumatatu asubuhi alirekodi taarifa na anazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Mjini akisubiri kufikishwa kortini.

Akithibitisha kukamatwa kwake, OCPD wa kituo cha polisi cha Mjini Bw Eliud Monari amesema, mshukiwa alikamatwa kufuatia video iliyosambazawa mitandaoni.

“Alionekana akimtesa mtu kwa kumpiga na kumchoma kwa moto na hii ilivutia kilio cha umma. Alikamatwa na yuko chini ya ulinzi wetu na anapaswa kukabiliwa na sheria,” Bw Monari amesema.

OCPD amesema bado wanatafuta ushahidi wa kutumia kortini hata wanapomtafuta mlalamishi.

Amesema kuwa video hiyo inayodaiwa ilirekodiwa mnamo Septemba 2020 na kwamba tukio hilo halikuripotiwa hadi wakati video hiyo imechipuka.

“Kutoka kwa habari ambazo tumepokea hadi sasa zinaonyesha kuwa tukio hilo lilitokea Ajab ndani ya Shimanzi. Tunafanya uchunguzi kabla ya mshukiwa kufikishwa kortini,” alisema.

Bw Monari amerai umma kutochukua hatua mkononi licha ya wao kuwa na nguvu ya kushinikiza kukamatwa kwa mshukiwa. Ametoa wito kwa wakazi kila wakati kuwakabidhi washukiwa kwa maafisa wa polisi badala ya kuchukua hatua mkononi.

“Mshukiwa alimdhulumu hata ikiwa alikuwa ametenda uhalifu. Hakufanya kulingana na sheria. Kuna njia nyingi za kughulikia washukiwa, kwa kuzingatia haki za kibinadamu,” Bw Monari alisisitiza.

Ameongeza kuwa korti zipo kudumisha haki na amewasihi raia wasitumie nguvu dhidi ya watuhumiwa.

You can share this post!

Onyo kwa wahudumu wa afya wanaoingiza ufisadi katika utoaji...

Mahangaiko ya Nakuru kuwa katika ‘lockdown’