• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Visa vya wanahabari kuendelea kuhangaishwa na maafisa wa polisi na raia vinatia hofu, mmoja Milele FM akiuguza majeraha

Visa vya wanahabari kuendelea kuhangaishwa na maafisa wa polisi na raia vinatia hofu, mmoja Milele FM akiuguza majeraha

Na SAMMY WAWERU

VYOMBO vya habari na wafanyakazi wake hasa watangazaji, waandishi na wapiga picha wamekuwa wenye mchango mkubwa kipindi hiki Kenya na ulimwengu unahangaishwa na janga la Covid-19.

Wamekuwa katika mstari wa mbele kuripoti yanayojiri, kuanzia visa vya maambukizi, maafa, waliothibitishwa kupona na mikakati iliyowekwa na serikali na wadauhusika kusaidia kudhibiti maenezi ya gonjwa hili ambalo ni kero la kimataifa.

Isitoshe, ni asasi ya kukusanya na kupasha habari ambayo imesaidia kulainisha serikali inapokosa na mtetezi mkuu wa haki ya wanyonge.

Sakata ya Covid Millionaires na iliyohusisha Mamlaka ya Usambazaji Dawa na Vifaa vya Kimataibabu Nchini (KEMSA) pamoja na baadhi ya maafisa wa idara ya afya, isingejulikana endapo vyombo vya habari visingejituma.

Ni kashfa iliyofukuliwa na kuangaziwa na runinga ya NTV, chini ya mwanahabari mpekuzi Dennis Okari.

Kimsingi, vyombo vya habari na wafanyakazi wake ni kati ya nguzo kuu katika kuboresha uchumi.

Licha ya bidii wanazotia, kuona kila mmoja amepashwa ujumbe kupitia magazetini, runinga, redio na pia tovuti za habari zinazomilikiwa na vyombo hivyo, waliotwikwa jukumu kukusanya habari hupitia kipindi kigumu hasa wanapokumbana na maafisa wa polisi na raia.

Si kisa kimoja, viwili au vitatu vimeripotiwa wanahabari kuhujumiwa na polisi.

Vinaendelea kushuhudiwa na vinaonekana kukita mizizi katika siku za hivi karibuni.

Tukio la hivi punde ni la mwanahabari wa Milele FM, kituo cha redio kinachopeperusha vipindi na matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili na kinachomilikiwa na Media Max Ltd, Bw David Omurunga ambaye alikamatwa na kushambuliwa Jumapili usiku, wakati akitekeleza majukumu yake.

Anauguza majeraha baada ya kutandikwa na maafisa wa polisi.

Ripota huyo wa Nakuru aliambia wanahabari kuwa aliingizwa kwenye gari la askari, akapitia unyama chini yao kabla ya kupelekwa katika kituo cha polisi cha Nakuru Central.

Bw Omurunga alisema alikamatwa baada ya saa mbili jioni, muda wa kafyu Nakuru, Nairobi, Kajiado, Machakos na Kiambu kuanza kutekelezwa, ambapo alikuwa akirekodi matukio.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza Machi 26, 2021 kukaza kamba sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti virusi vya corona, katika kaunti hizo tano.

Maeneo hayo, kafyu ya kitaifa inatekelezwa kati ya saa mbili jioni hadi saa kumi alfajiri.

Vilevile, kaunti hizo na ambazo zimetajwa kuwa hatari kwa maambukizi ziliwekewa zuio la kuingia na kutoka.

“Walinishambulia licha ya kujitambulisha kuwa mimi ni mwanahabari (kupitia kitambulisho cha kazi, kinachotolewa na baraza la kusimamia vyombo vya habari na wanahabari nchini – MCK). Nilipata kichapo na kuuguza majeraha,”mwandishi huyo akasimulia, akitambua walivyokuwa baadhi ya maafisa.

Ni tukio la dhuluma ambalo limekashifiwa vikali na MCK, ikimtaka Inspekta Mkuu wa Polisi, IG Hillary Mutyambai kuchukulia hatua za kisheria maafisa wahusika.

“Waandishi wa habari ni miongoni mwa wafanyakazi wa huduma za dharura, waliorodheshwa na serikali. Sijajua ni kwa njia gani maafisa wa polisi wamejitwika jukumu la kutengeneza sheria, badala ya kuzitekeleza. Tunamhimiza Inspekta Mutyambai ahakikishe haki kwa mwanahabari aliyeshambuliwa imepatikana, uchunguzi ufanywe na wahusika waadhibiwe kisheria,” akasisitiza Bw David Omwoyo, afisa mkuu mtendaji wa MCK.

Cha kushangaza, kulingana na ripota aliyeshambuliwa Nakuru alisema askari waliohusika walimsuta “wanahabari hujifanya kama waliosoma sana na sisi (maafisa wa polisi) tutawatuliza”.

Ni matamshi ya dharao na kudunisha asasi ya upashaji habari, ambayo maafisa haohao wanaitegemea kupata habari muhimu kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.

Hali kadhalika, ni maafisa haohao hukimbilia wanahabari wanaponyanyaswa na mwajiri wao, na pia kutetea haki zao za kimsingi.

Kisa cha Jumapili, si cha kwanza wanahabari kuhujumiwa.

Machi 2021, katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Londo Nakuru, wanahabari walishambuliwa na raia wakati wakifuatilia zoezi hilo.

Ni aibu na fedheha kuona wanaoitwa kupeperusha na kupasha taifa kuhusu takwimu za maambukizi ya Covid-19, wakihangaishwa na idara ya usalama.

Serikali inadai kutambua uwepo wa wanahabari nchini, ila haiwalindi.

Kenya ni nchi inayothamini demokrasia, na waandishi wanapohangaishwa wakati wanatekeleza majukumu yao wananyimwa haki yao Kikatiba, kwa mujibu wa kipengele cha 35, ambacho kimeweka wazi haki ya kupata taarifa popote pale.

You can share this post!

Joash Onyango atawazwa mchezaji bora wa mashabiki wa Simba...

Mamake Tecra jinsi mamilioni yake yalipelekewa Omar Lali