• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Mkopo wa IMF wazua hasira kwa Wakenya

Mkopo wa IMF wazua hasira kwa Wakenya

Na MARY WANGARI

MKOPO wa Sh257 bilioni uliopewa serikali ya Kenya wiki jana na Shirika la Fedha Duniani (IMF) umepingwa na Wakenya ambao wamekasirishwa na ukopaji wa kila mara wa utawala wa Jubilee.

Wakenya waliojawa na hasira walilalamika kuwa mikopo hiyo, ambayo sasa imegonga Sh8 trilioni ni tisho kwa uhuru wa kitaifa.

Katika hatua iliyoashiria wananchi walivyochoka na usimamizi wa uchumi, baadhi ya Wakenya jana walianzisha harakati za kukusanya saini kwa lengo la kushinikiza IMF kufutilia mbali mkopo huo mpya.

“Acheni kutoa mikopo hiyo kwa sababu inaporwa na watuy wenye nguvu serikalini. Serikali haitumii hela hizo kusaidia wananchi. Sisi Wakenya tunalemewa na mzigo mzito wa madeni haya. Hatuwezi kuyalipa, hivyo acheni kutupatia,” akasema Dkt Peter Ogallo.

Baadhi walishangaa ni vipi IMF ilikubali kuipatia Kenya mkopo, hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukiri hadharani kuwa Sh2 bilioni zinaibwa katika serikali yake kila siku.

“Rais alirekodiwa peupe akisema Sh2 bilioni hupotea kila siku na hawezi kufanya chochote,” alisema Brian Obonyo.

Kuna wale walitilia shaka uadilifu wa IMF wakihoji kuwa shirika hilo linachangia kuendeleza ufisadi nchini.

Akizungumza na Taifa Leo jana, mtaalamu wa uchumi Dkt David Ndiii alisema japo raia wana haki ya kuelezea hisia zao, IMF ina mkataba wa kimataifa na Kenya kama taifa mwanachama ambao unaongozwa na kanuni maalum.

Kulingana na mtaalamu huyo, ni Bunge la Kenya pekee linaloweza kusaidia raia na wala si taasisi nyinginezo za kigeni.

“Wakenya wamekosa imani na taasisi zao na wanaelekeza hasira zao kwa mashirika ya kigeni wakitaka ziwasaidie. Ikiwa huwezi kupata msaada kutoka kwa serikali yako basi hakuna kwingine unakoweza kupata usaidizi,” akasema Dkt Ndii.

You can share this post!

Uhuru ashauriwa kuiga Kibaki

Zaidi ya wafungwa 1,800 watoroka baada ya shambulio la...