• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
TAHARIRI: Watoto walioacha shule watafutwe

TAHARIRI: Watoto walioacha shule watafutwe

KITENGO CHA UHARIRI

RIPOTI zinazidi kutokea kuhusu idadi ya wanafunzi waliokosa kufanya mitihani ya kitaifa ya shule za msingi na upili (KCPE na KCSE) mtawalia mwaka huu 2021.

Wakati shule zilipofungwa kwa karibu mwaka mzima wa 2020 kwa sababu ya janga la virusi vya corona, wataalamu walitabiri kuwa idadi ya wanafunzi ambao wangeacha shule ingeongezeka ikilinganishwa na jinsi ilivyokuwa miaka iliyopita.

Hata hivyo, badala ya hatua kuchukuliwa kuhusu ripoti za utafiti zilizokuwa zikifanywa, kwa mfano kuhusu mimba za mapema na matumizi ya dawa za kulevya, baadhi ya maafisa serikalini waliamua kupuuzilia mbali ripoti hizo.

Kufikia sasa, serikali haijatoa ripoti rasmi kamili kuhusu idadi ya watoto ambao hawakurudi shuleni wakati zilipofunguliwa kuelekea mwishoni mwa mwaka uliopita hadi baadaye Januari mwaka huu.

Lakini ripoti chache zinazotolewa na walimu na maafisa wengine wa maeneo ya mashinani, zinaonyesha taswira ya jinsi mambo yalivyo.

Mbali na wanafunzi walioathirika kwa mimba za mapema, kuolewa wakiwa hawajakamilisha elimu, na athari za mihadarati, kuna wengine waliojitosa katika biashara wakakataa kurudi shuleni baada ya kuonja utamu wa pesa kidogo wanazopata.

Haya ni masuala ambayo ni lazima yajadiliwe na yatafutiwe suluhisho ili kuokoa kizazi hiki kisije kikapotoka.

Ni sharti Wizara ya Elimu pamoja na wadau wengine wakuu wa sekta hiyo watafute jinsi wanafunzi wote waliokatiza masomo yao, hasa katika kipindi hiki cha janga la corona, watawezeshwa kurudi shuleni ili wakamilishe elimu.

Katiba imeeleza wazi kuwa elimu ya msingi ni haki ya kila mtoto, hivyo basi haifai serikali ivumilie mtu yeyote ambaye atajaribu kuvuruga haki hii kwa watoto wetu kwa njia yoyote ile.

Hatua zitakazotafutwa zisiwe za kulenga watahiniwa waliotarajiwa kufanya mitihani ya mwaka huu pekee, bali wanafunzi wa madarasa yote ambao hawakurudi shuleni.

Umuhimu wa elimu si jambo ambalo linafaa kuchukuliwa kwa mzaha, bali utiliwe mkazo wakati wote.

Ili kufanikisha nia ya kuwarudisha watoto hao shuleni, itahitajika wadau wote washirikiane kuhusu suala hili kwa minajili ya kulinda maslahi ya watoto nchini.

You can share this post!

Tumieni pesa za refarenda kulisha raia – wabunge

ODONGO: Tiketi ya ODM: Oparanya, Joho wanajipumbaza tu!