• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
WANGARI: Serikali ihakikishe kuna oksijeni ya kutosha hospitalini

WANGARI: Serikali ihakikishe kuna oksijeni ya kutosha hospitalini

Na MARY WANGARI

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe majuzi alilamikia kuhusu uhaba wa hewa ya oksijeni, hali ambayo ni kikwazo kikuu dhidi ya juhudi za kuangamiza Covid-19.

Waziri huyo aliwalaumu baadhi ya Wakenya wanaohodhi mitungi 20,000 ya oksijeni manyumbani kwao na kuwasihi kuirejesha viwandani.

Kwa sasa, ni asilimia 16 pekee ya hospitali za umma zilizo na hewa hiyo muhimu inayotumika kwa wagonjwa mahututi, kulingana na taarifa mpya kutoka kwa jopokazi la Wizara ya Afya la kupambana na Covid-19.

Japo Kenya inajivunia viwanda 75 vya kuunda oksijeni, ni jambo la kuhofisha kuwa si vyote vinavyofanya kazi kwa sasa, hasa wakati huu ambapo makali ya virusi vya corona yamezidi kuchacha.

Haya yanajiri huku mahitaji ya oksijeni katika vituo vya afya yakiongezeka kwa kasi huku Kenya ikikabiliana na wimbi la tatu la mkurupuko wa janga hilo.

Kiwango cha maambukizi nchini kilikuwa kimefikia asilimia 26 huku idadi ya walioambukizwa ikipanda hadi 131, 116, kulingana na takwimu zilizotangazwa na Wizara ya Afya wiki jana.

Wataalam wamekadiria kuwa kiwango cha oksijeni kinachohitajika katika hospitali nchini huenda kikafikia tani 880 hivi karibuni.

Hii ni ongezeko kwa kiasi kikubwa cha tani 320 katika kipindi cha miezi mitatu tu kutoka tani 560 mnamo Januari mwaka huu.

Katika kipindi sawa mwaka jana, kiwango cha oksijeni kilichohitajika kwa shughuli za matibabu katika vituo vya afya nchini kilikuwa tani 410.

Mkondo huu ni wa kutisha hasa baada ya bosi wa Wizara ya Afya kukiri kuwa viwanda vilivyopo haviwezi kutosheleza kiwango cha mahitaji ya oksijeni kinachozidi kuongezeka.

Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo 2017 liliorodhesha oksijeni kama dawa muhimu kwa matibabu ya maradhi yanayosababisha viwango vya chini vya oksijeni kwenye damu.

Miaka miwili baadaye, Kenya ilifuata mkondo kwa kujumuisha oksijeni katika Orodha ya Dawa Muhimu Nchini.

Iliorodhesha oksijeni kama mojawapo wa dawa sita nyeti za kuwezesha mgonjwa kupumua na ambazo zinastahili kupatikana katika vituo kutoka viwango vya zahanati.

Umuhimu wa kuwepo oksijeni ya kutosha katika vituo vyote vya afya nchini hauwezi ukasisitizwa vya kutosha iwapo tuna nia ya kufanikisha juhudi za kupiga vita kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Ikiwa ni mwaka mmoja tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kilipotangazwa Kenya, ukosefu wa kipengele hicho muhimu mno katika juhudi za kukomesha gonjwa hilo unadhihirisha utepetevu na kutowajibika kwa kiasi kikubwa.

Inakadiriwa kuwa serikali inahitaji Sh2bilioni ili kuweza kusambaza hewa hiyo muhimu katika vituo vya afya zaidi ya 300 kote nchini.

Ni sharti serikali na wadau husika ihakikishe kuwepo kwa mahitaji yote ya kimsingi ili kuimarisha juhudi za kukabiliana na Covid-19.

[email protected]

You can share this post!

ODONGO: Tiketi ya ODM: Oparanya, Joho wanajipumbaza tu!

Mwalimu mkuu akamatwa Machakos kwa kusambaza mtihani wa...