• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
Wakenya waomboleza rais wa mchezo wa kuogelea Kenya (KSF) Patrick Muyah

Wakenya waomboleza rais wa mchezo wa kuogelea Kenya (KSF) Patrick Muyah

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Mchezo wa Kuogelea Kenya (KSF) na Wakenya kwa jumla wanaomboleza kifo cha rais wa shirikisho hilo Patrick Muyah aliaga dunia mnamo Jumanne saa mbili na nusu asubuhi.

Kupitia mtandao, KSF imethibitisha kifo chake Jumanne jioni ikisema, “Ni kwa huzuni mkubwa tunawajulisha kumpoteza Patrick K. Muyah. Rambirambi zetu zifikie familia na rafiki zake. Muyah alitumikia mchezo wa kuogelea kwa zaidi ya miaka 30. Kujitolea kwake na huduma zake katika mchezo huu nchini Kenya kunatambulika na tutamkosa sana.”

Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya uogeleaji ya Kenya, Malik Mwabondo aliomboleza mwendazake Muyah akisema “Ni siku ya huzuni mkubwa kwa mchezo wa kuogelea humu nchini”.

Marehemu Muyah alihudumu katika Kamati Kuu ya KSF kwa karibu miaka 20. Kabla ya kifo chake, Muyah alikuwa ametumikia KSF kama kaimu rais kwa miaka mitatu. Kenya kwa sasa inatumikia marufuku kutoka kwa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA) kutokana na mivutano ya uongozi. Mipango ya mazishi ya Muyah haijatangazwa. Ripoti zinasema alikata roho kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona vinavyohangaisha dunia nzima.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Majitaka, uchafuzi wa Ziwa Nakuru...

Mwanamume aliyeonekana akiteswa kwa kuchomwa na chandarua...