Wanaoenda kuhiji Mecca kuhitaji cheti cha chanjo

CECIL ODONGO na AFP

VIONGOZI wa Kiislamu nchini wameeleza wasiwasi kuhusu uwezekano wa waumini kukosa kupokea chanjo dhidi ya virusi vya corona haraka iwezekanavyo, baada ya serikali ya Saudi Arabia kutangaza kuwa watu waliopokea chanjo pekee ndio wataruhusiwa kushiriki hija mwaka huu 2021.

Utawala wa kifalme wa nchi hiyo mnamo Jumatatu ulitangaza kwamba kila atakayesafiri kutimiza nguzo hiyo ya tano ya Kiislamu atahitajika kuwa na cheti cha kuchanjwa virusi vya corona.

Hajj ya mwaka 2021 inatarajiwa kuanza Julai 20 hadi Julai 24, kulingana na mwandamo wa mwezi.

Mwaka 2020 ibada hiyo iliyumbishwa pakubwa kufuatia kukithiri kwa maambukizi ya corona ulimwenguni.

Kando na hali ya wasiwasi ambayo imekuwepo nchini kwamba chanjo inayotolewa na serikali haitoshi wananchi wote, viongozi hao walisema wananchi wengi wamechanganyikiwa kuhusu aina ya chanjo iliyo bora.

Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK), Sheikh Bini, aeleza kuwa japo mtu anafaa kupokea chanjo kwa hiari, ni lazima mahujaji waikumbatie ili kufanikisha safari yao.

“Safari hiyo ya ibada ni manufaa sana kwa kila muumini na ni vyema wachanjwe. Hata hivyo, serikali inafaa kutoa mwelekeo ili watu wasiwe na tashwishi kuhusu chanjo inayotolewa,” akasema Sheikh Bini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Ushauri wa Waislamu ( KEMNAC), Sheikh Juma Ngao, alisikitishwa na jinsi utoaji chanjo umeanza kuingizwa siasa.

“Serikali itahitaji kuhamasisha raia na pia kuamua ni chanjo ipi inafaa. Kwa sasa zoezi hilo muhimu la afya limeingizwa siasa; imebuka kwamba kuna pande mbili – Naibu Rais na chanjo yake, kisha serikali na chanjo nyingine. Hili lishughulikiwe haraka kuwaondolea raia hofu,” akasema Sheikh Ngao.

Mwenyekiti wa Baraza la Waumini wa Kiislamu (Supkem), Hassan Ole Naado, naye alisema wataelekeza mahujaji kuhusu suala la chanjo baada ya kupokea mawasiliano rasmi kutoka Saudia.

Wizara ya Hajj na Umrah nchini humo ilisema kupitia taarifa kuwa, ni makundi matatu ya watu wataidhinishwa kuwa “wamepokea chanjo”.

Wanajumuisha wale ambao wamepokea dozi mbili za chanjo, wale watakaokuwa wamepokea dozi moja angalau siku 14 kabla ya hija, na watu ambao wamepona kutokana na maambukizi hayo.

Ni watu hao pekee ndio wataruhusiwa kushiriki umrah, pamoja na kuhudhuria sala kwenye Msikiti Mkuu katika mji mtakatifu wa Mecca.

Sera hiyo itawezesha “kupandisha kiwango cha utendakazi” cha Msikiti Mkuu wakati wa Ramadan, ilisema wizara hiyo.

Iliongeza kuwa masharti hayo pia yatazingatiwa kabla ya kuingia Msikiti wa Manabii katika mji mtakatifu wa Medina.

Wizara ilisema sera hiyo itaanza na Ramadan, ambayo inatazamiwa kung’oa nanga mwishoni mwa mwezi huu, lakini haikueleza kanuni zitadumu kwa muda upi.

Aidha, haikufafanua iwapo sera hiyo, ambayo imeanzishwa wakati visa vya maambukizi ya corona vimeongezeka mno katika ufalme huo, itaendelezwa kwa haji ya kila mwaka itakayofanyika baadaye mwaka huu.

Saudi Arabia imeripoti visa zaidi ya 393,000 na vifo 6,700 kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hatari vya corona.

Wizara ya Afya ilisema kuwa imetoa zaidi ya dozi milioni tano za chanjo ya corona katika taifa hilo lenye watu zaidi ya milioni 34.

Tangazo hilo lilijiri baada ya Mfalme Salman kumbadilisha waziri wa hajj mwezi uliopita, chini ya mwaka mmoja baada ya taifa hilo kuandaa kusanyiko ndogo zaidi la hajj katika enzi za sasa sababu ya jnga hilo linalokumba ulimwengu.

Ni Waislamu 10,000 pekee wakazi wa Saudi Arabia waliruhusiwa kushiriki; idadi chache zaidi ikilinganishwa na Waislamu 2.5 milioni kutoka kote duniani walioshiriki 2019.

Mohammad Benten aliachishwa kazi na wadhifa wake kutwaliwa na Essam bin Saeed, kulingana na tangazo la kifalme lililochapishwa na kituo rasmi cha habari nchini humo.

Mwishoni mwa Julai mwaka uliopita, ufalme huo ulipokea idadi ndogo zaidi ya watu waliohudhuria hija, ambayo ni mojawapo wa nguzo za dini ya Kiislamu, na ambayo ni lazima kwa kila Mwislamu aliye mzima kiafya kushiriki angalau mara moja maishani mwake.

Ni Waislamu 10,000 pekee ambao ni wakazi wa Saudi Arabia walioruhusiwa kushiriki idadi ambayo ni chache zaidi ikilinganishwa na Waislamu 2.5 milioni kutoka kote duniani walioshiriki 2019.