Suluhu aunda kamati ya kuchunguza corona TZ

ROSEMARY MIRONDO na ELIZABETH EDWARD

DAR ES SALAAM, Tanzania

RAIS Samia Suluhu Hassan alisema Jumanne kuwa ananuia kuunda kamati ya wataalam watakaochunguza kwa njia ya kitaalam janga la Covid-19 na kuishauri serikali yake kuhusu hatua inazopaswa kuchukua.

“Ninakusudia kuunda kamati ya wataalamu waliangalie suala la corona kwa upana halafu watushauri sisi Serikali, watupe upeo wa tatizo hili lilivyo na hayo yanayopendekezwa na ulimwengu.

“Hatuwezi kujitenga kama kisiwa wala hatuwezi kupokea yanayoletwa bila kufanya utafiti,” alisema Rais Suluhu.

Kulingana naye, Tanzania inahitaji mtazamo wazi na unaoeleweka kuhusu janga hilo ili ifanye maamuzi ya busara.

Ili kufanikisha hayo, alisema kuwa Tanzania haiwezi ikategemea ripoti kutoka nje kuhusu hali ya mkurupuko huo huku taifa hilo likiwa halina ripoti zozote.

“Tanzania inahitaji kuwa na uelewa wake binafsi kuhusu ni wapi tumesimama kuhusiana na suala la Covid-19,” alisisitiza.

Tanzania ilitangaza mara ya mwisho data kuhusu Covid-19 karibu mwaka mmoja uliopita ambapo wakati huo data hiyo iliashiria kuwa nchi hiyo ilikuwa na visa 509.

Tangu wakati huo, serikali ilianza kuchukua msimamo kuwa Tanzania haina Covid-19 huku ikihimiza raia kutumia matibabu ya kienyeji kama vile kujifukiza kwenye mvuke.

Wakati huo huo, Rais Suluhu aliitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa na kuagiza maafisa husika wasitumie kifua kuvidhibiti.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu wa makatibu wakuu, aliagiza wizara husika kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinafuata sheria na taratibu zilizowekwa.

“Ninasikia kuna vyombo vya habari mlivifungia, vifungulieni na vifuate sheria tusiwape mdomo kwamba tunamnyima uhuru wa kuzungumza. Tusiwafungie kibabe, wafungulieni na kuhakikisha wanafuata kanuni na miongozo ya Serikali.”

“Watakapofanya makosa, adhabu zitolewe kulingana na jinsi sheria inavyoelekeza, waacheni wafanye kazi yao isionekane wanazuiwa kuongea,” alisema.

Aidha, aliagiza wizara hiyo ambayo inahusika vilevile na michezo, sanaa na utamaduni, ikiwemo usimamizi wa haki za wasanii na wanamichezo, kuhakikisha wasanii hao wananufaika kwa kazi zao.

Kwa takribani miaka mitano sasa, leseni za vyombo vya habari Tanzania, hasa magazeti, za kuchapisha na kusambaza, zilisitishwa kwa muda huku mashirika mengine yakitakiwa kuomba upya leseni hizo.