MAKALA MAALUM: Majangili wenye silaha kali wazidi kuhangaisha wakazi wa Kerio Valley

FLORAH KOECH na BARNABAS BII

SERIKALI ilipositisha kwa muda operesheni ya kupokonya silaha wakazi wa kaunti zilizosheheni visa vya ukosefu wa usalama Kaskazini mwa Bonde la Ufa ili kutoa nafasi ya mazungumzo, wakazi walikuwa na matumaini makubwa ya kupata amani ambayo ingewaletea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kuimarisha maisha yao kwa jumla.

Lakini mwezi mmoja baadaye, watu kutoka jamii za wafugaji zinazopigana wanaendelea kujikusanyia silaha hatari za kuwazidi maafisa wa usalama waliotumwa eneo hilo kukabiliana na mizozo inayosababishwa na wizi wa mifugo na vitendo vya ujangili.

Maelfu ya bunduki na risasi zinaendelea kuingizwa katika Bonde la Kerio huku uhasama baina ya jamii za wafugaji ukizidi kushuhudiwa; ishara kwamba magenge ya wahalifu yanapanga mashambulizi.

“Kinachofanyika ni kwamba wahalifu wenye silaha hawakutii agizo la serikali la kusalimisha silaha haramu na kutoa nafasi ya mazungumzo ili kutafuta amani ya kudumu.

“Badala yake baadhi yao wanaendelea kununua silaha kali. Mzozo huu sasa sio kuhusu wizi wa mifugo au vitendo vya ujangili, lakini wahalifu wamebadilisha mbinu kulenga biashara na kuiba mali,” alisema Chetotum, mkazi wa Kapedo.

Juhudi za kutafuta amani eneo hilo zilipata pigo mwishoni mwa wiki wakati wavamizi waliokuwa na silaha walishambulia maeneo ya Arabal na Mochongoi katika kaunti ndogo ya Baringo Kusini na kuiba mifugo zaidi ya 200.

Kamishna wa Kanda ya Rift Valley, Bw George Natembeya, akithibitisha kisa hicho alisema kwamba, milima na mabonde katika eneo hilo imetatiza operesheni ya kuwasaka majangili hao na kupata mifugo walioibwa.

“Kundi letu la maafisa wa usalama liko huko na limeanza kuwasaka majangili hao likitokea upande wa Kaunti ya Samburu,” alifichua Bw Natembeya.

Baadhi ya majangili wanaofanya mashambulizi Kapendo – kwenye mpaka wa kaunti za Baringo na Turkana – huwa wanatoroka kuelekea Kaunti ya Pokot Magharibi na kisha kuvuka mpaka hadi nchini Uganda wanakojificha miongoni mwa jamaa zao kabla kurejea nchini baada ya serikali kusitisha operesheni ya kutwaa silaha kutoka kwa wakazi.

Jamii ya Pokot hupatikana katika mataifa ya Kenya na Uganda na ni kawaida kwao kuvuka mpaka kutafuta malisho na maji kwa mifugo wao katika nchi hizo mbili.

“Tunachojua ni kwamba baadhi ya wahalifu hawa wanajificha katika Bonde la Suguta au wako Pokot Magharibi wakielekea Uganda,” alisema Gavana wa Baringo Stanley Kiptis na kuitaka serikali kukabiliana vikali na wahalifu hao.

Eneo la Bonde la Kerio ni makazi ya jamiii za Pokot, Turkana, Marakwet, Tugen, Illchamus na Samburu ambazo zimekuwa zikipigana kwa muda mrefu.

Serikali ilisimamisha zoezi la kupokonya wakazi silaha lililoanzishwa miezi miwili iliyopita katika maeneo hatari ya Tiaty Mashariki, Tiaty Magharibi na Turkana Mashariki kufuatia visa vya mashambulizi vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu 10 mwezi Januari, wakiwemo maafisa wa usalama wa ngazi za juu.

Mamia ya maafisa wa usalama walitumwa katika maeneo hayo matatu kutwaa silaha haramu za wakazi, kutafuta mifugo walioibwa na kukamata wahalifu wenye silaha wanaohangaisha wakazi.

Maeneo yaliyolengwa kwa zoezi hilo ni Ameyan, Paka, Silale, Nadome, Komolion, Kapau, Toplen, Mukutani, Chesitet, Nakoko, Riong’o, Lomelo, Lokori na Kapedo ambako mashambulizi hutokea kila wakati.

Tangazo la kusimamisha operesheni hiyo ili kutoa nafasi ya mazungumzo lilitolewa na Bw Natembeya kwenye mkutano wa amani, uliofanyika katika hoteli ya Lake Begonia Spa Resort mwaka jana.

Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi wa kisiasa, kidini na pia wataalamu kutoka jamii za Pokot wanaoishi Tiaty na Pokot Magharibi.

“Tunasimamisha operesheni hii kwa muda wa mwezi mmoja mlivyoomba ili kuwapa nafasi mzungumze na wakazi ili wasalimishe silaha haramu na kufurusha wahalifu.

“Iwapo mbinu hii haitafaulu, basi mtushauri njia bora ya kuitekeleza, lakini tunajua viongozi waliochaguliwa wako na uwezo wa kushawishi wakazi,” alisema Bw Natembeya.

Kulingana na Gavana Stanley Kiptis (Baringo) na mwenzake Profesa John Lonyangapuo (Pokot Magharibi), suluhu kutoka kwa wakazi itazaa amani ambayo inahitajika sana katika kaunti hizo zinazopambana na ujangili Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Prof Lonyangapuo aliomba serikali kusitisha operesheni hiyo kwa muda wa mwezi mmoja ili viongozi na wadau kutoka jamii ya Pokot wazungumze na wakazi kutafuta njia mwafaka ya kuwashawishi majangili kusalimisha silaha zao.

“Hatuna uwezo wa kuwapokonya silaha wahalifu kwa sababu ndio walituchagua. Lakini tunajua mbinu tunazoweza kutumia kuwafikia katika maficho yao na kisha wasalimishe silaha ndani ya mwezi mmoja. Shabaha yetu ni kumaliza desturi hii ya kale na kuwasihi majangili kupeana silaha hizo kwa serikali,” alieleza Gavana huyo.

Wabunge Mark Lomunokol (Kacheliba), David Pkosing (Pokot Kusini), Peter Lochakapong (Sigor) na Gladwell Cheruyot walisisitiza haja ya kuimarisha hali ya kiuchumi ya wafugaji kwani ndiyo njia bora zaidi ya kuwafanya kuachana na mila zilizopitwa na wakati, kama vile wizi wa mifugo.

Walisema kwamba kuwapokonya silaha wakazi wa eneo hilo lililokithiri visa vya ujangili hakutamaliza uhalifu huo wala wizi wa mifugo, ila ni kwa kuleta miradi ya maendeleo kwa jamii hizo ambazo zimetengwa kwa muda mrefu.

Alieleza Bw Lomunokol: “Hilo la kutwaa silaha kwa nguvu litaishia kulemaza uchumi wa eneo hili ambalo bado liko nyuma kimaendeleo. Ni watu wasio na hatia watateseka huku wahalifu wakienda mafichoni.

“Tukumbatie mbinu nyingine za kupata silaha hizo kutoka kwa majangili bila kuwatia hatarini wakazi wasio na hatia na kuwasababishia mateso.”

Hata hivyo, mambo hayajabadilika chini ya mwezi mmoja baada ya mkutano huo wa amani.

Eneo linashuhudia wimbi jipya la mashambulizi ambayo yamelazimisha familia nyingi kutoroka makwao na mali kuibwa.