WASONGA: Mvutano wa Kenya, Uingereza kuhusu Covid haustahili

Na CHARLES WASONGA

NIPE nikupe kati ya Kenya na Uingereza kuhusu kanuni za kuzuia msambao wa virusi vya corona ikomeshwe haraka, kwani ni tisho sio tu kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili bali ya kibiashara.

Kenya na Uingereza ni washirika wakuu katika nyanja za biashara na uwekezaji.

Kwa mfano, kuna zaidi ya kampuni 100 za asili ya Uingereza zimewekeza nchini Kenya, na hivyo hutoa nafasi za ajira kwa Wakenya.

Kulingana na Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu nchini (KNBS), Kenya iliuza bidhaa za thamani ya Sh40 bilioni nchini Uingereza mnamo 2019, nyuma ya Uholanzi ambako Kenya iliuza bidhaa za thamani ya Sh48 bilioni.

Katika mwaka huo, kampuni za Uingereza ziliwekeza mali ya thamani ya Sh118.7 bilioni nchini Kenya.

Kwa kuwa Uingereza haijatangaza ni lini itaondoa marufuku ya watu kutoka Kenya kuingia humo, biashara nyingi zitaathirika.

Moja ya biashara hizo ni safari za angani za shirika la ndege la Kenya Airways, ambalo mwaka jana liliandikisha hasara ya Sh36.2 bilioni.

Kulingana na data kutoka Wizara ya Masuala ya Kigeni, Uingereza ni soko kubwa kwa mazao ya kilimo kutoka Kenya; kama vile chai, kahawa, maua, mboga na matunda.

Mnamo 2019 Kenya ilitia kibindoni Sh20.9 bilioni kutokana na mauzo ya mazao hayo nchini Uingereza.

Isitoshe, ni majuzi tu ambapo mabunge ya Uingereza na Kenya yaliidhinisha Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) kati ya mataifa hayo mawili – wa thamani ya Sh200 bilioni kwa mwaka.

Kwa mfano, chini ya mkataba huo wa EPA maua, mboga na matunda kutoka Kenya hayatatozwa ushuru katika masoko ya Uingereza. Bila shaka wakulima wa mazao hayo kutoka Kenya watafaidi pakubwa.

Ingawa marufuku ya sasa haijaathiri ndege za mizigo, inapaswa kuondolewa haraka iwezekanavyo kwani itachafua mazingira ya kibiashara kati ya Kenya na Uingereza.

Uingereza inafaa kuondoa Kenya katika orodha ambayo raia wake hawaruhusiwi huko, ikiwa ni kweli kwamba ilichukua hatua hiyo kutokana na ongezeko la maambukizi ya Covid-19.

Data kuhusu Covid-19 zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi nchini Kenya ni asillimia 17 kwa wastani.

Lakini kiwango cha maambukizi katika mataifa kama Amerika ni asilimia 54, Ujerumani asilimia 60 na Canada asilimia 32.

Kinaya ni kwamba Uingereza haijajumuisha mataifa haya kwenye orodha ya nchi ambazo raia wake wamepigwa marufuku kuingia humo.

Kwa upande mwingine, ingawa Kenya imeweka masharti makali dhidi ya watu wanaotoka Uingereza kuingia nchini ili kuzuia msambao wa corona, hatua hiyo ichukuliwe kwa njia isiyoonekana kama kulipiza kisiasa.

Japo, ni wajibu wa serikali hizi mbili kulinda raia wao dhidi ya kuambukizwa corona, hazifai kufanya hivyo kwa njia itakayoathiri mahusiano ya kibiashara na kidiplomasia.

Habari zinazohusiana na hii