NGILA: Heko AU kuunda teknolojia ya pasipoti za kidijitali

Na FAUSTINE NGILA

JE, unafahamu kuwa safari zote za ndege sasa zinawalazimu wasafiri kuwa na pasipoti ya corona kando na ile ya kawaida?

Mataifa yaliyoendelea yalikuwa ya kwanza kuleta mfumo huu lakini sasa bara la Afrika limekumbatia teknolojia mpya ya pasipoti za kidijitali.

Ni mtindo ambao utaendelea kutumika katika viwanja vya ndege kote duniani, hata iwapo maambuziki mapya ya corona yatapungua.

Kwa hili, mataifa ya Afrika, licha ya kukosa kuhusika katika juhudi za kuunda chanjo ya corona, raundi hii yamekuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza kuunda pasipoti ya kidijitali kwa kutumia teknolojia yake yenyewe.

Kampuni za ndege za Afrika tayari zimeanza kukumbatia teknolojia hiyo, iliyoundwa na Umoja wa Afrika (AU) kurahisisha usafiri, katika kipindi ambapo safari za ndege zimelemazwa na ukosefu wa vipimo na vyeti vya corona.

Kampuni za Kenya Airways na Ethiopian Airlines zimeungana na Shirikisho la Usafiri wa Angani Afrika Magharibi na Kati (ASKY) kutumia mfumo wa kidijitali wa PANABios, unaoendeshwa na AU ikishirikiana na Vituo vya Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC).

Jukwaa hilo la kidijitali kwa jina Trusted Travel Pass, litawezesha abiria kuthibitisha vipimo vyao na vyeti vya corona kwa haraka kabla ya kupanda ndege, ithibati kuwa Afrika sasa imekomaa kiteknolojia na inaweza kujitegemea.

Ingawa teknolojia za mabara mengine bado zipo, AU imeonekana kuwa mstari wa mbele kuhamasisha mataifa yote kutumia teknolojia hiyo kama njia moja ya kusaidia kampuni za ndege barani kujipa mapato wakati huu mgumu kibiashara.

Wateja sasa wanafurahia safari za angani bila bughudha wakitumia pasipoti za kidijitali, kwani zimewawezesha maafisa katika viwanja vya ndege kutambua iwapo abiria wamechanjwa na iwapo wametimiza masharti ya kudhibiti virusi vya corona.

Binafsi nimependezwa na jitihada hizi za AU kuhakikisha kuwa bara la Afrika lina mtandao wake wa kuthibitisha vipimo vya corona kupitia kwa maabara, hali ambayo inahakikisha biashara inaendelea kama kawaida miongoni mwa mataifa ya Afrika.

Kwa mara ya kwanza, Waafrika tumeungana kukataa teknolojia za ughaibuni ambazo gharama yake iko juu sana, na kujikubali kwamba tuna ubunifu wa kutosha kupambana na changamoto zetu wenyewe.

Hata hivyo, baadhi ya mataifa bado yanazembea kuchangamkia jukwaa hilo, hata wakati yanafahamu fika kuwa vyeti vya corona vya kidijitali vinahitajika iwapo taifa linafanya biashara ya uchukuzi wa angani.

Mataifa hayo yanapaswa kukoma kutilia shaka mfumo huo kwani umeundwa kwa kiwango cha kimataifa, kuwajali Waafrika wote bila ubaguzi, na kutokomeza ufisadi katika sekta ya afya huku ukipunguza gharama ya vipimo vya maabara.

Cha muhimu ni kuwa huu ni mfumo ambao utatusaidi kukusanya data yetu binafsi itakayotuwezesha kufanya maamuzi ya kibiashara haraka, kando na mazoea ya mabara mengine kukama data katika uchumi wa Afrika bila hata kulipia senti.

Iwapo mfumo huo wa PANABios utatumiwa na mataifa yote; utaboresha usimamizi wa sera kote Afrika na kuinua biashara baina ya mataifa; kupiga jeki utalii, uwekezaji na utamaduni; na hatimaye kuhakikisha Afrika haiachwi nyuma katika maendeleo.

Habari zinazohusiana na hii