Mwanawe Haji atawazwa Seneta mpya wa Garissa bila kupingwa

Na CHARLES WASONGA

NI rasmi sasa kwamba Abdulkadir Mohamed Haji ndiye Seneta mpya wa Kaunti ya Garissa kuchukua nafasi ya babake, marehemu Yusuf Haji, baada ya kutawazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kwenye notisi katika Gazeti Rasmi la Serikali toleo la Aprili 6, 2021 mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alitangaza kuwa kiti hicho hakitawaniwa katika uchaguzi wa debeni kwani ni mgombeaji mmoja aliyejitokeza.

“Kwa kuzingatia mamlaka yaliyoko kwenye vipengele vya 88 (4) na 98 (1) vya Katiba ya Kenya na sehemu husika za sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na Sheria ya Uchaguzi, 2011, tume inatangaza yule mmoja aliyeidhinishwa kuwania kiti hiki kuwa Seneta Mteule wa Kaunti ya Garissa,” Bw Chebukati akasema.

Abdulkadir Mohamed, maarufu kama Abdul Haji, alikuwa mwaniaji wa wadhifa huo kwa tiketi ya chama cha Jubilee.

Kufikia Alhamisi wiki jana ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa wagombeaji kuwasilisha stakabadhi zao za uteuzi kwa IEBC, hakuna mgombeaji mwingine alikuwa amefanya hivyo isipokuwa Abdul Haji.

Bw Haji aliidhinishwa na IEBC Jumanne wiki jana baada ya kuwasilisha karatasi zake za uteuzi kwa Afisa Msimamizi wa Uchaguzi kaunti ya Garissa Bw Hussein Gure katika Chuo Anuai Kitaifa cha North Eastern, mjini Garissa.

Mnamo Alhamisi, afisa huyo akasema hivi: “Baada ya kupokea karatasi za uteuzi kutoka kwa mgombeaji mmoja pekee, nimewasilisha habari hiyo kwa makao makuu ya IEBC ili tume ifanye uamuzi.”

Bw Haji alipata uidhinishwaji kutoka wa koo za Abduwak, Aulihan na Abdalla kwamba ndiye anayefaa kuchukua nafasi ya babake kama seneta.

Koo hizo tatu zina ushawishi mkubwa katika siasa za Garissa.

Mwanasiasa huyo chipukizi pia alipata uungwaji mkono kutoka chama cha Orange Democratic Movement (ODM), chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto na muungano wa One Kenya Alliance unaoshirikisha vinara wa vyama vya ANC, Ford Kenya, Wiper na Kanu.

Haji sasa anasubiri kuapishwa rasmi Seneti itakaporejelea vikao vyake mnamo Mei 11, 2021.