Dume bwege labururwa na mke

Na JOHN MUTUKU

HURUMA, NAIROBI

KALAMENI aliyekuwa ametoroka mkewe na wanawe watatu na kupiga kambi katika nyumba ya kimada wake, aliaibika mkewe alipomvamia, akamkamata pabaya na kumburura hadi nyumbani watu wakitazama.

Inadaiwa polo huyo alikuwa amemtoroka mkewe wa ndoa yao, na kuelekeza mshahara wake wote kwa kimada wake.

Pia ilidaiwa alitumia kiasi kikubwa cha pesa kumfungulia hoteli mwanadada huyo.

“Niliolewa na mtu au niliolewa na mnyama! Huyu ni mwanamume mwenye akili timamu? Anawezaje kuwaacha wanawe na kuenda kwa mwanamke mwengine? Kesho ninashuka kwenye hoteli hiyo. Nitawavuruga kinoma,” mke aliapa. Siku iliyofuatia, mke wa kalameni huyo alijiandaa na kuelekea kwenye hoteli. Alimpata mumewe na kimada wake wakiendelea kufanya biashara.

“Hapa ndipo nyumbani kwako? Kama sipo, wafanya nini hapa? Je, unajua wanao walishindaje au walilalaje?” alimuuliza mumewe. Jamaa alibaki bila maneno.

“Yaani, huyu ni nani amekuja kunifukuzia wateja?” kimada aliuliza kwa dharau.

Mke wa kalameni alimrukia na kumtandika makofi mazito mazito. Alinyakua chapati na mandazi na kurusharusha ovyo barabarani.

“Njoo, nifuate nikupeleke kwa wanao,” mke aliruka na kuukamata ‘mpini’ wa kalameni. Aliukamata sawasawa na kwa nguvu hivi kwamba hakuna chochote ambacho kalameni angefanya ila kuinua mikono ishara ya kusalimu amri.

Walienda hivyo, mke mbele akivuta mpini, kalameni nyuma akimfuata, maumivu yakimwandama kweli. Walipofika kwenye ploti, mke alimwachilia na kumsukuma ndani ya nyumba akimsindikiza kwa makofi.

“Na iwe siku ya mwisho kwenda kwa hawara huyo. Ikitukia siku nyingine, nasikitika utajuta,” mke alionya. Siku hizi, kalameni amepoa na kutulia nyumbani.