• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Kalonzo asema ndiye mfaafu zaidi kuwania urais chini ya One Kenya Alliance

Kalonzo asema ndiye mfaafu zaidi kuwania urais chini ya One Kenya Alliance

Na MWANGI MUIRURI

KIONGOZI wa chama cha Wiper Democratic Movement – Kenya, Kalonzo Musyoka amesisitiza Jumatano kuwa yeye ndiye mfaafu zaidi kuteuliwa kuwania urais na muungano wake mpya wa One Kenya Alliance unaojumuisha Musalia Mudavadi wa ANC, Gideon Moi wa Kanu na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya.

Akiwa katika mahojiano na runinga ya Citizen, Bw Kalonzo ameashiria kuwa mvutano unaweza ukatokea katika harakati za kusaka mwaniaji wa urais katika muungano huo ikizingatiwa kuwa Mudavadi na Moi nao wameapa kuwa liwe liwalo watakuwa wakiwania wadhifa huo.

Bw Kalonzo alisema kuwa atakuwa akiwania Urais lakini mikakati ya kuteua mpeperushaji bendera ikimwendea kombo na aangukie pua, “nitakubali na maisha iendelee mbele japo sioni hilo likitokea.”

Akipata urais, amesema siku 100 zake za kwanza madarakani atapambana na ufisadi kwa dhati na Wakenya watamuelewa kuwa hatakuwa na mzaha, pia apige jeki maisha ya Wakenya ili yainuke na waondolewe mzigo mkubwa wa mahangaiko ya madeni na umaskini.

Amekana dhana kwamba Rais Uhuru Kenyatta ndiye nguvu fiche zinazosukuma muungano wao mpya lakini akasema “ikiwa ana nia ya kujiunga nasi tuko tayari kumpokea.”

Hata hivyo, amesema kuwa hadhani kuwa kwa sasa “huo ndio mjadala tunaofaa kujihusisha nao kwa kuwa Rais ana kazi yake kwa sasa ya kujenga kumbukumbu yake ya kustaafu.”

Amesema kuwa hata hakumbuki mara ya mwisho alipoongea na rais Kenyatta, lakini akikasirikia swali kwamba ikiwa sio rais Kenyatta anayewaunga mkono ndani ya muungano huo, kama kuna uwezekano kuwa walio na nguvu kupindukia za kiserikali wakipewa jina la majazi la Deep State ndio wanawaunganisha kwa nia ya kumtenga Bw Odinga.

Bw Kalonzo amesema dhana ya ‘Deep State’ kwa kawaida huwa na uhusiano mkuu na Kamati Kuu ya Kiusalama—National Security Council—ambapo Rais ndiye mwenyekiti na Naibu Rais akiwa ndiye naibu mwenyekiti.

“Sasa unataka kusema kwamba tunaungwa mkono hata na Naibu Rais ambaye ametangaza nia yake ya kusukuma ajenda ya Uhasla Kenya hii kwa kuwa hata yeye ni Deep State?” akahoji.

Amesema kuwa Kenya ni nchi ya mabasi mbadala ya kuwania uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano na sio maajabu kuhepa Nasa au wao wenyewe kuhepwa.

Amesema kuwa hakuna la kuchambuliwa kama lisilo la kawaida kuona washirika wa zamani kisiasa wakitengana au kuja pamoja.

“Hata awali tushawahi kuwa na mpango kama Pentagon ambao ulikuwa wa kuunda muungano wa Cord na ambao leo hii ni historia iliyozikwa ndani ya kaburi la sahau,” akaeleza.

Bw Kalonzo amesema kuwa “kwa sasa mimi na wengine tuko tayari kudhibiti muungano wetu mpya na tuusukume tukiujenga hadi uwe na makali ya uwaniaji 2022.”

Amesema kuwa muungano wake unaunga mkono refarenda kuhusu BBI iandaliwe kabla ya Julai ndio Wakenya waamue au wakatae na taifa lisonge mbele.

Mradi mfu

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa ODM na mwandani wa Bw Odinga tayari amesema kuwa refarenda katika mazingara ya Covid-19 na madeni kupindukia sio suala la dharura sasa, hivyo basi kuzua mjadala wa ikiwa BBI ni mradi mfu kwa sasa.

Bw Oparanya alisema kuwa haifai Wakenya wakiwa na ugumu huu wote wa makali ya janga la ugonjwa kuingizwa katika refarenda Julai na mwaka 2022 mwezi wa nane waingie katika uchaguzi mkuu, hali zote zikihitaji bajeti kubwa.

Bw Kalonzo ameshikilia kuwa “huu sio wakati wa kuachana na mkondo wa BBI kwa kuwa inawezekana tuambatanishe hali hizo zote mbili ziende sambamba—kupambana na Covid-19 na pia kuendeleza mchakato wa BBI hadi refarenda.”

Huku ikionekana wazi kwamba huenda msukumo wake wa BBI ni kupata mpangilio mpana wa kugawana nyadhifa ili kuwaunganisha pamoja kama vinara ndani ya muungano huo, amekana kuwa hiyo ndiyo nia yake.

Amesema kuwa sio lazima kuwe na BBI ndipo wabaki wakiwa wameungana kama muungano akisema kuwa hata wakiunda Nasa hakukuwa na nyadhifa za ziada za kuahidiwa lakini waliafikiana kwamba Bw Odinga akiwa Rais, yeye angekuwa naibu wake, Bw Mudavadi akiwa mshirikishi wa Baraza la Mawaziri naye Wetang’ula akiwa naibu wa Mudavadi—kumaanisha eneo la Magharibi lingekuwa na Waziri Mkuu na naibu wake—hali ambayo labda ni hadaa, kwa mujibu wa wachanganuzi kadha.

You can share this post!

Dume bwege labururwa na mke

Umuhimu wa usawa wa kijinsia kielimu katika kupunguza...