Mwili wa aliyemuuza ng’ombe Sh130,000 wapatikana umezikwa kwa kinyesi cha ng’ombe

Na MWANGI MUIRURI

MUDA wa saa chache baada ya Bw Kinyua Macharia kumuuza ng’ombe wake kwa Sh130,000 amepatikana Jumatano akiwa maiti na mwili wake kuzikwa kwa kinyesi kinachoaminika ni cha ng’ombe uyo huyo, mita chache kutoka boma lake kijijini Kabati, Kandara, Kaunti ya Murang’a.

Hadi sasa, maafisa wa polisi wanajaribu kusaka aliyemuua, nia yake na alikokimbilia kwa kuwa hadi sasa hajanaswa huku jamaa na marafiki wa mwendazake wakiitaka idara ya polisi kutatua kitendawili cha mauaji hayo.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Mohammed Barre, mshukiwa hadi sasa ni kitwana aliyekuwa katika familia hiyo mwenye asili ya nchi jirani, Uganda, na ambaye hadi sasa ametoweka na virago vyake.

“Shida kubwa katika uchunguzi huu ni kwamba haijulikani aliyemuua alikuwa akilenga nini kwa kuwa pesa hizo zote za mauzo ya ng’ombe huyo zimepatikana zikiwa katika akaunti yake ya M-Pesa na pia simu yake kupatikana nyumbani kwake,” akasema Bw Barre.

Kando na mwili wake kulikuwa na nyundo ambayo inaaminika ilitumika kama silaha ya kumuua kabla ya mwili wake kubururwa hadi kwa shimo lililochimbwa nyuma ya zizi la ng’ombe na ukazikwa kwa kinyesi cha ng’ombe.

Majirani waliokuwa na majonzi makuu wamemtaja mwendazake kama mtu wa bidii katika kusaka riziki na waliyemtambua kwa jina Kinyua wa Macharia.

“Mwili ulikuwa na majeraha kichwani na tumeupeleka mochari kuhifadhiwa na bila shaka utafanyiwa upasuaji na uchunguzi mwingine wa kimaabara kubainisha hali na mazingira halisi ya mauaji hayo,” akasema Bw Barre.

Amesema kuwa wapelelezi kwa sasa wanawinda mshukiwa huyo aliyekuwa akifanya kazi katika boma hilo na ambaye tangu asubuhi hajaonekana katika kijiji hicho.

Ajabu ni kwamba, hakuna habari kumhusu kitwana huyo huku Bw Barre akiwataka wenyeji wawe makini sana wanapotoa ajira katika mashamba, makazi au sehemu za biashara “kwa kuwa huu mtindo wa kuwapa wageni kazi bila ya kuwahoji na kuwafahamu zaidi kumekuwa changamoto kuu katika usalama wa eneo hili.”

Hata hivyo, Bw Barre ameahidi kuwa kila aina ya mbinu itatekelezwa kunasa mshukiwa au washukiwa waliotekeleza mauaji hayo.