Kimunya adokeza huenda bunge likaitwa kujadili ripoti ya mswada wa BBI

CHARLES WASONGA na MWANGI MUIRURI

BUNGE la Kitaifa litafanya kikao maalum wiki ijayo kujadili ripoti kuhusu mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Kiongozi wa wengi Amos Kimunya alisema Jumanne ana imani kwamba Kamati ya Pamoja ya Wabunge na Maseneta ambayo ilikuwa ikishughulikia mswada huo itawasilisha ripoti yake wiki hii.

“Nafahamu fika kwamba kamati ya pamoja itawasilisha ripoti yake katika afisi yangu Alhamisi au Ijumaa. Baada ya hapo nitaitisha kikao maalum cha Bunge la Kitaifa ili tuusukume mswada wa BBI hatua nyingi,” akasema kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen jioni.

Bw Kimunya ambaye ni Mbunge wa Kipipiri aliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufanya maandalizi hitajika ili Wakenya waweze kushiriki kura ya maamuzi mwishoni mwa Mei au mwanzoni mwa Juni.

“IEBC inaweza kufanya kura ya maamuzi Mei au Juni 2021. Kile kinachohitajika ni kwa tume hiyo kutenga siku 21 za kampeni ambazo zitaendeshwa kwa njia ya utulivu wakati huu wa janga la Covid-19,” akasema.

Akaeleza: “Hatujachelewa zaidi jinsi inavyosemekana huko nje. Kura ya maamuzi inaweza kufanyika jinsi ilivyoratibiwa.”

Kwa mujibu wa sheria za bunge, nambari 29 kiongozi wa wengi na mwenzake wa wachache wana uwezo wa kumwandikia Spika wa Bunge kumwomba aitishe kikao maalum “endapo kuna suala la dharura na lenye umuhimu wa kitaifa ambalo linafaa kujadiliwa.”

Wiki jana kamati ya pamoja bunge la kitaifa na seneti kuhusu haki na masuala ya sheria iliteua watalaamu wawili wa masuala ya sheria kuwasaidia kutanzua suala la iwapo bunge la kitaifa na seneti yanaweza kuufanyia marekebisho mswada wa BBI au la.

Wataalamu waliopewa kibarua hicho ni Profesa Patricia Kameri-Mbote na Mhadhiri wa somo la Uanasheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi Collins Odote.

Kimunya ameshikilia Jumatano ameshikilia kwamba referenda kuhusu mpango wa maridhiano ya kitaifa (BBI) inawezekana hata Mei 2021.

“Mbali na Julai jinsi wanavyosema wengi, hata mwezi ujao (Mei) inawezekana tuandae hii refarenda. Hakuna cha kusingizia kwa kuwa inawezekana,” amesema Kimunya aliye pia Mbunge wa Kipipiri aliyepokezwa afisi hiyo baada ya kutimuliwa kwa Bw Aden Duale aliyesemwa kuwa na imani ya kisiasa kwa Naibu Rais Dkt William Ruto.

Dkt Ruto hajakumbatia BBI licha ya kwamba amekataa katakata kuongoza mrengo wa kupinga akisema kuwa hatajihusisha na refarenda kwa kuwa sio suala la kupewa kipaumbele.

Akijibu maswali katika mahojiano na runinga ya Inooro, Bw Kimunya amesema kuwa amehakikishiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Sheria na Haki kwamba atapata ripoti wakati wowote kuanzia Alhamisi ikiangazia namna ya kuhakikisha refarenda hiyo inafanyika.

“Nikiipata, sitakuwa na lingine la kufanya ila tu tukiwa na Spika tutaliita bunge ambalo kwa sasa liko katika likizo na tujadiliane kuhusu uidhinishaji wa mswada wa BBI kupelekwa kwa wananchi wakaupigie kura,” akasema.

Bw Kimunya alisema kwamba Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haina la kuizuia kuzindua mikakati ya kuandaa referenda “kwa kuwa inajua kwa uhakika kwamba ule mswada uliopitishwa na mabunge ya Kaunti ndio tulipokezwa na kisheria hakuna tutakachobadilisha hivyo basi tangu utoke kwa ugatuzi wangekuwa wameanza kuuandalia mikakati ya referenda.”

Alisema kuwa kuna baadhi ya watu wanajaribu kuleta viziki vya kila aina akisema “BBI ni wazo ambalo ni lazima liafikiwe kwa hali na mali.”

Matamshi ya Bw Kimunya sasa yanazua masuala nyeti ambayo yamekuwa yakiangaziwa na wengi nchini—kuhusu busara ya kuwatuma Wakenya kwa kura ya refarenda kukiwa na changamoto ya janga la Covid-19 na pia maadili ya kutumia zaidi ya Sh10 bilioni kuandaa refarenda hiyo wakati Wakenya wengi wanalala njaa na kupoteza riziki katika mahangaiko ya uchumi uliofungwa minyororo ya utumwa wa madeni kupindukia.

Hata hivyo, Bw Kimunya alisema kuwa hakuna cha kuzua wasiwasi kwa kuwa “serikali inajizatiti kukabiliana na hali zote jinsi zinavyochipuka.”

Pia, matamshi ya Bw Kimunya yanazua uwezekano wa mtafaruku zaidi ambapo kuna wanasiasa ambao wameshikilia kuwa bunge linafaa kupewa nafasi ya kubadilisha vipengele tata ndani ya BBI huku wengine wakitaka referenda iahirishwe hadi baada ya uchaguzi wa 2022.

Aidha, kuna kesi mahakamani za kupinga referenda hiyo na ambapo tayari IEBC imezimwa na ilani ya mahakama isithubutu kunadaa zoezi hilo kabla ya kesi kutatuliwa, lakini Bw Kimunya sasa akisema kunafaa kuzinduliwa mikakati ya kura hiyo—ikimaanisha aidha anajua uamuzi wa mahakama utakuwa gani, au kuna njama ya kuiandaa bila kuzingatia wajibu wowote wa mahakama.

Imekadiriwa kuwa mchakato huo wote wa BBI utagharimu taifa zaidi ya Sh35 bilioni huku utekelezaji kwa upana wake wote ukigharimu Wakenya jumla ya Sh361 bilioni.