• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Afisa wa GSU amuua mkewe kisha naye ajitoa uhai

Afisa wa GSU amuua mkewe kisha naye ajitoa uhai

Na SAMMY WAWERU

INSPEKTA Mkuu wa Polisi Nchini, IG, Hillary Mutyambai ameongoza idara yake kuwaomboleza maafisa waliofariki Jumanne jioni.

Afisa Hudson Wakise wa kitengo cha kukabiliana na ghasia (GSU) aliripotiwa kumuua mke wake, Pauline Wakasa wa kitengo cha trafiki, kwa kumpiga risasi mara kadha, kisha akajitoa uhai.

Kwenye taarifa ya Bw Mutyambai kwa vyombo vya habari mnamo Jumatano, kisa hicho cha kikatili kilitokea Jumanne katika makazi ya maafisa hao yaliyoko nje ya kambi ya GSU, Ruaraka, Nairobi.

“Idara ya Polisi inathibitisha kifo cha Hudson Wakise wa nambari ya usajili kikosini 99047 na mke wake Pauline Wakasa, 98615 kufuatia mzozo unaoonekana kuwa wa kinyumbani, kilichotokea jana (Jumanne) jioni,” IG Mutyambai akasema kupitia taarifa.

“Wakise alikuwa mlinzi katika Wizara ya Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali ya Kitaifa, mke wake naye alikuwa afisa wa trafiki kituo cha polisi cha Kilimani,” akaelezea.

Kulingana na IG, Wakise alikuwa amechukua likizo ya mapumziko mafupi Aprili 1, 2021 na alirejea kazini Jumatatu alasiri, mwendo wa saa tisa.

“Inakisiwa alimuua mke wake kwa kumpiga risasi, kabla ya kujitoa uhai kwa bunduki. Walioshuhudia na majirani wanasaidia maafisa wa polisi kwa uchunguzi, kufuatia tukio hilo lililofanyika nje ya kambi ya GSU (katika makazi yao) saa kumi na moja za jioni,” Bw Mutyambai akasema, akiomboleza maafisa hao na kutuma salamu za pole kwa familia zao.

Wakise alikuwa mlinzi wa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i.

You can share this post!

Kimunya adokeza huenda bunge likaitwa kujadili ripoti ya...

VITUKO: Bawabu amgeuzia mwalimu mkuu kibao cha wizi wa...