• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Bunge la kaunti lafungwa kuepusha ueneaji corona

Bunge la kaunti lafungwa kuepusha ueneaji corona

Na COLLINS OMULO

BUNGE la Kaunti ya Nairobi jana Jumanne liliahirisha vikao vyake hadi wakati usiojulikana kufuatia kuongezeka kwa visa vya Covid-19.

Madiwani sita wamelazwa hospitalini huku wawili wakipigania maisha yao kwenye mitambo wakiwa katika hali mahututi.

Hatua hiyo imejiri baada ya madiwani 40 kupatikana na virusi hivyo hatari baada ya kufanyiwa vipimo huku wengine wapatao 15 wakikabiliana na gonjwa hilo.

Wiki mbili zilizopita, Rais Uhuru Kenyatta aliomba madiwani wa kaunti tano zilizofungwa wasitishe vikao vya ana kwa ana kwa muda, sawa na bunge la taifa.

Bunge la Nairobi lilikuwa ndio mwanzo tu limerejelea vikao vyake jana asubuhi baada ya likizo ya wiki mbili iliyoanza Machi 18, 2021.

Wakipitisha Mswada wa Kuahirisha Bunge hilo hadi wakati usiojulikana, madiwani wa kaunti hiyo walikubali kuwa Covid-19 imeenea katika bunge hilo hivyo pana haja ya kuahirisha vikao vyake hadi maambukizi yatakapopungua.

Akitoa mswada huo, Kiongozi wa Wengi katika bunge hilo Abdi Guyo, alisema alikuwa ndipo tu amepona kutokana na Covid-19 ambayo ilikuwa imewaathiri vilevile, jamaa wa familia yake. Diwani huyo wa Wadi ya Matopeni/Springvalley alisema bunge hilo sasa litasitisha vikao vyake hadi taarifa nyingine itakapotolewa wakati visa hivyo vitakapopungua.

“Gonjwa hili ni hatari na tunatilia maanani maagizo ya Rais. Wengi wetu tumekuwa wahasiriwa wa gonjwa hili. Sasa hivi madiwani wetu wawili wamelazwa katika hali mahututi ambapo zaidi ya wengine 40 wamepatikana na virusi hivyo,” alisema Bw Guyo.

Akiunga mkono mswada huo, Kiongozi wa Wachache Michael Ogada alisema hakuna chochote kinachostahili kuzidi maisha ya watu kwa umuhimu na kwamba likizo hiyo ni muhimu ili kuchunguza jinsi gonjwa hilo linavyosambaa.

“Hakuna kilicho na umuhimu kama maisha na sisi kuja hapa kutaathiri maisha. Virusi hivi vimekatiza maisha. Tuchukueni likizo na kuzingatia kanuni za Wizara ya Afya,” alisema diwani wa huyo wa Embakasi.

Spika Benson Mutura alisema kamati za Bunge hilo zinaweza kuendelea kukutana kielektroniki ikiwa kuna shughuli muhimu itakayowasilishwa kwao.

“Ninapendekeza sasa kusitisha vikao vya Jumanne na Alhamisi na vikao vingine vyovyote ambavyo huenda vikajitokeza, kama vile kamati, vitafanyika kielektroniki,” alisema Bw Mutura.

Bunge hilo limekuwa likishiriki vikao vyake mara mbili kila Jumanne na Alhamisi.

You can share this post!

Matokeo ya KCPE kutolewa mwezi huu

Muungano wa makanisa chini ya mwavuli wa FEICCK walaani...