• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 3:17 PM
Jinsi NMS inavyojikakamua kuangazia usalama wa waendao kwa miguu jijini

Jinsi NMS inavyojikakamua kuangazia usalama wa waendao kwa miguu jijini

Na SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Kuboresha Huduma za jiji la Nairobi (NMS) limekuwa likimiminiwa sifa kwa kazi ya kipekee.

Si mara moja, mbili au tatu Rais Uhuru Kenyatta amenukuliwa akilipongeza.

Mwaka 2020 katika mojawapo ya ziara ya mitaa Nairobi, kiongozi huyo wa nchi alilisifia kutokana na jitihada zake kuangazia upungufu wa maji.

“Chini ya muda mfupi, tumeona vile NMS imetatulia wakazi wa Nairobi tatizo sugu la ukosefu wa maji. Kwa sasa, mingi ya mitaa iliyofaidika kupitia miradi ya shirika hili itakuwa ikipata maji ya bure, bila kulipa ada yoyote. Awali, wakazi walikuwa wakinunua mtungi mmoja wa maji wa lita 20 kwa Sh50, lakini mahangaiko hayo yameisha,” alisema Rais Kenyatta.

NMS ikiwa chini ya uongozi wa Meja Jenerali Mohamed Badi, Rais anasema imemsaidia kuafikia baadhi ya ahadi zake kwa wakazi wa Nairobi.

Shirika hilo lilizinduliwa Machi 18, 2020, kipindi ambacho aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Bw Mike Mbuvi Soko alikuwa anaendelea kuandamwa na sakata za ufisadi, ubadhirifu wa fedha na mali ya umma, na matumizi mabaya ya ofisi.

Bw Sonko hata hivyo alibanduliwa Desemba 2020 na madiwani wa Kaunti ya Nairobi, uamuzi wao baadaye ukatiwa muhuri na bunge la seneti.

Kwa sasa, Nairobi inaongozwa na Naibu Gavana, Bi Anne Kananu, ambaye alikuwa ameteuliwa awali na Sonko ila hakuwa ameanza kazi wakati akiwa (Sonko) mamlakani.

Bi Kananu aliapishwa kuingia afisini Januari 2020, licha ya uteuzi wake kuwa na pingamizi.

Huku NMS ikiendelea kumiminiwa kongole, japo haikosi wakosoaji, kuna huu mradi wa kuimarisha barabara za jiji.

Hakika, shirika hilo linahitaji kupongezwa kutokana maendeleo hayo.

Mfano, mojawapo ya barabara iliyo pembezoni mwa City Market inaashiria utendakazi bora wa NMS.

Sehemu maalum ya waendao kwa miguu katikati mwa mojawapo ya barabara eneo la City Market, jijini Nairobi, iliyojengwa na NMS. Picha/ Sammy Waweru

Ina sehemu maalum ya waendao kwa miguu, katikati mwa barabara, ambapo watu hutembea kwa utulivu, kinyume na awali ambapo walihangaika kufuatia msongamano unaoshuhudiwa kandokando mwa barabara.

Ikiwa inalaki wanaotoka katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), mwishoni mwa daraja la kuelekea au kutoka UoN, ni rahisi kutembea kwa miguu, kufuatia sehemu hiyo maalum bararabani bila kukwaruzana na magari.

Ni sehemu kati ya nyinginezo jijini Nairobi, ambazo wakazi wataishi kuikumbuka NMS.

Meja Badi akiwa alichomolewa kutoka kikosi cha kijeshi nchini (KDF), Rais Kenyatta alisema akimaliza kuhudumia Nairobi, atarejea jeshini ila kwa sasa amepewe fursa achape kazi.

“Meja Jenerali si mwanasiasa, ni mfanyakazi wa umma ambaye nilimpa majukumu…” Rais Kenyatta wakati mmoja akanukuliwa akimsuta Bw Sonko, na ambaye alidai Meja Badi aliteuliwa kuhujumu utendakazi wake kama gavana.

Miradi aliyotekeleza afisa huyo wa kijeshi na mingine inayoendelea na ijayo, ni ishara Kenya inaweza kuimarika, baadhi wakitamani shirika kama hilo lizinduliwe katika kaunti zote nchini.

Kikwazo cha maendeleo nchini ni tamaa za waliochaguliwa au kuteuliwa kushikilia nyadhifa za umma, ambapo wakikalia viti wanakasata ufisadi vilivyo.

Wanasahau kuwa wamekabidhiwa majukumu hayo na wananchi, ambao ni walipa kodi na ushuru, unaopaswa kuwafanyia maendeleo kama vile kuwaimarishia barabara, huduma za afya, masomo, miongoni mwa nyinginezo.

You can share this post!

Diwani ndani miaka minane kwa kujaribu kuokoa watu...

Hasira za raia zashtua serikali