• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
KINYUA BIN KING’ORI: ODM, Raila watajilaumu wenyewe wakipigwa chenga

KINYUA BIN KING’ORI: ODM, Raila watajilaumu wenyewe wakipigwa chenga

Na KINYUA BIN KING’ORI

KARATA kali ya kisiasa inasubiri chama cha ODM na kiongozi wake Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Ukweli ni kwamba kuna baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa katika serikali ya Jubilee ambao hawampendi Odinga.

Baadhi yao wako karibu na Rais Uhuru Kenyatta na hawaoyeshi dalili za kumpenda kinara huyo, iwe sirini au hadharani.

Hata wandani wengine wa Rais hawajakumbatia ushirikiano wake na Odinga – almaarufu Handisheki – wakiwemo wafuasi katika ngome yake ya Mlima Kenya.

Namna mambo yamekuwa yakiendelea siku za hivi majuzi, ni bayana hakuna uaminifu wa kujivunia tena kati ya Jubilee ya Kenyatta na ODM ya Odinga.

Licha ya vigogo hao wawili majuzi kuonekana wakitembea pamoja kukagua maendeleo Nairobi na Kajiado, lisilofichika ni kwamba Handisheki ni sawa na kitumbua kilichoingia mchanga.

Kwa sasa viongozi hao wanataka kuficha uhasama wowote ili BBI ipite maana imebeba maslahi yao kisiasa 2022.

Kama ilivyo kawaida ya wasaliti kisiasa, Odinga ameshindwa kusoma nia ya Rais na wandani wake.

Raila Odinga awe atakuwa debeni 2022 kuwania urais au la, ajue Handisheki ilikuwa tu ngazi ya Rais Kenyatta kuhakikisha amefanikiwa kumtuliza na kuzima upinzani ili awe na mazingira tulivu ya kumaliza kipindi chake cha pili bila usumbufu au serikali yake kuhangaishwa na upinzani.

Kwa hivyo, aliyefaidi Handisheki pakubwa ni Rais. Tangu mapatano hayo, amekuwa akifanya mabadiliko serikalini kuteua wanasiasa wa ODM, Wiper na ANC katika nyadhifa mbalimbali.

Hata wabunge wa upinzani pia wameteuliwa kuongoza kamati muhimu Bungeni.

Hayo yote yamefanikiwa kwa sababu ya Odinga kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta.

Hata hivyo, kuna watu serikalini wanahofia Odinga kuingia ikulu kumrithi Kenyatta. Wanapanga mikakati na njama kila uchao kuzima nyota ya kinara huyo wa ODM ili umaarufu wake uwe umesambaratika kabla ya 2022.

Uoga na hofu yao ndiyo imeleta usaliti katika Handisheki. Ni kikundi hicho tu kinahusika na mikakati ya kumzima na kumsaliti Naibu Rais William Ruto.

Ni hao bado wamejitokeza tena kufaulisha usaliti wa Odinga na kumfungia mlango wa Ikulu.

Wafuasi wengi wa Odinga wanasadiki kuwe nuru au giza lazima “Baba” ataungwa mkono na Rais Kenyatta 2022 akiwania urais. Ikiwa Odinga atapata upendeleo wa Rais kweli atakuwa kifua mbele.

Rais naye kwa ujanja wake amekuwa akijitokeza kumpoesha kila wafuasi wake wanapolalamika.

Utakumbuka madai ya hivi juzi kwamba kuna watu wameteka mchakato wa BBI na kumtupa kapuni Raila Odinga.

Rais Kenyatta akajitokeza kumpigia simu na hata kukutana naye ambapo alimhakikishia BBI itaendelea.

Yote tisa, ukweli ni kwamba kuna njama mmoja wa viongozi wa muungano wa One Kenya Alliance kupewa njuga za BBI na hata kupendelewa na Rais mwenyewe kukalia kigoda cha Ikulu 2022.

Ingawa Rais hajatangaza msimamo wake juu ya nani atapendelea kumrithi si ajabu Raila Odinga hatakuwa mmoja wao.

Inasadikiwa Raila Odinga ni mwanasiasa mweledi, mahiri na mjanja katika kupanga mikakati ya kisiasa.

Sasa anafaa kutambua mapema mbinu faafu kwake kutegua mitego na njama dhidi yake ikiwemo kuhujumu na kufifisha umaarufu wa chama cha ODM katika maeneo ambayo amekuwa akipata uungwaji mkono kama pwani na magharibi.

You can share this post!

TAHARIRI: Huduma za polisi zijumuishe ushauri

KAMAU: Mikopo: Tushaingia mtego wa China na Magharibi