• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
KAMAU: Mikopo: Tushaingia mtego wa China na Magharibi

KAMAU: Mikopo: Tushaingia mtego wa China na Magharibi

Na WANDERI KAMAU

JE, Rais Uhuru Kenyatta anajali mustakabali wa Kenya?

Anajali maslahi ya vizazi vijavyo?

Je, angependa vizazi hivyo viishi katika nchi huru au inayohangaishwa na mataifa ya kigeni kutokana na msururu wa madeni?

Ni maswali ambayo yameibuka baada ya Wakenya kulalamikia hatua ya serikali kukopa Sh255 bilioni kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani (IMF) “kuendeleza mikakati ya kupambana na janga la virusi vya corona.”

Kwa ghadhabu, Wakenya wameanzisha kampeni kali kwenye mitandao ya kijamii, wakilirai shirika hilo kutoikopesha Kenya fedha hizo, kwani hawajaona manufaa yoyote kutoka kwa mikopo kama hiyo iliyotolewa awali kwa serikali.

Bila shaka, hii ni mara ya kwanza kwa Wakenya kuungana kuonyesha ghadhabu yao dhidi ya mtindo wa serikali ya Rais Kenyatta kuendelea kukopa mabilioni ya pesa kutoka kwa taasisi za kifedha duniani.

Cha kushangaza ni kuwa, katika wakati huu wote ambao Kenya imeingia kwenye mtego wa madeni ya kimataifa, Rais Kenyatta amekuwa akitoa hakikisho kwamba kila kitu ki shwari.

Naam, hajakuwa akionyesha wasiwasi wowote kuwa baada yake kung’atuka uongozini mwaka ujao, yeye hataubeba mzigo wa kuyalipa bali atakiachia kizazi kitakachokuwepo kuendelea kukabiliana nao.

Kufikia sasa, Kenya ina deni la nje la zaidi ya Sh8 trilioni.

Katika makadirio ya bajeti mwaka huu, Kenya itatumia karibu Sh1 trilioni kulipia madeni inayodaiwa na nchi tofauti na mashirika mbalimbali ya kifedha kama vile IMF, Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kati ya taasisi zingine.

Katika simulizi ambazo zimekuwepo kuhusu uhalisia wa madeni ya kitaifa, ni hatua ya Rais Kenyatta na washirika wake kupuuzilia mbali uwezekano wa Kenya kushindwa kulipa madeni hayo.

Kati ya nchi zinazotudai deni lake kubwa zaidi ni China. China ni mfadhili wa baadhi ya miradi mikubwa zaidi nchini, kama vile Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Nairobi hadi Mombasa.

China ina historia ya kutwaa mali na himaya za baadhi ya nchi zinazoshindwa kulipia madeni yake. Baadhi ya nchi ambazo zimejikuta hapo ni Sri Lanka na Zambia.

Mnamo 2019, China ilitwaa usimamizi wa Bandari ya Hambantota, Sri Lanka, baada ya taifa hilo kushindwa kulipa baadhi ya mikopo iliyokuwa imepewa na China.

Chini ya makubaliano kati ya mataifa hayo mawili, China itasimamia shughuli za bandari hiyo kwa miaka 99 ijayo!

Nchini Zambia, China inadaiwa kuchukua udhibiti wa Uwanja wa Kitaifa wa Ndege wa Zambia, Shirika la Kitaifa la Utangazaji la Serikali na Shirika la Kitaifa la Zambia la Kusambaza Umeme (ZESCO) “ili kujilipa deni lake” baada ya Zambia kushindwa kulipa madeni iliyokopeshwa.

Bila shaka, mikopo hii imegeuka kuwa ukoloni-mamboleo katika karne hii ya 21.

Cha kusikitisha ni kuwa, tunaonekana kutojali tunakoelekea!

Tunaonekana kutofahamu kuwa tayari, tumeingiza guu moja kwenye ujanja wa China kunyakua baadhi ya mali ya nchi yetu.

Kampeni za mitandaoni hazitafaa! Wakenya waamke waseme yametosha!

[email protected]

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: ODM, Raila watajilaumu wenyewe...

Avuliwa taulo sababu ya visura