Avuliwa taulo sababu ya visura

Na JOHN MUTUKU

KARIOBANGI, Nairobi

JUMBE za mapenzi ambazo jamaa alitumiwa na ‘mipango ya kando’ nusura zivuruge ndoa mkewe alipoziona na kumkabili vikali.

Polo, ambaye hakuwa na mazoea ya kuacha simu mezani akienda kuoga, alijuta kwa kuisahau siku hiyo.

Mkewe alikuwa akimshuku kwa muda mrefu, na alipata fursa ya kuchukua simu akatoka nayo nje ya nyumba kusoma arafa.

“Hani, mbona waniacha kwenye baridi ukisingizia ni lockdown? Umeniacha nile nini pamoja na wanao?” ujumbe mmoja ulisema.

“Uliahidi kufika kwangu leo usiku. Unajua kafyu inaanza saa mbili. Hakikisha umewasili saa moja na nusu. Nitakuwa nikikusubiri mpenzi,” arafa ya mwanamke mwingine ilimtetemesha mke wa polo.

“Mpenzi, mbona siku hizi umeadimika hivyo? Au ni kafyu imekufanya kuganda kwa huyo shosh wako unayemwita mkeo? Nataka zawadi za Pasaka mie na wanangu. Usipozinunua, kwangu usionekane; najua ujanja wako,” SMS ya mpenzi wa tatu ilimvunja moyo kabisa.

Polo alipotoka bafuni hata mke hakumpa nafasi ya kujifuta maji. Alimvamia na kumpokonya taulo kabla kuanza kumtupia makofi.

“Loma mkubwa wewe! Kumbe badala ya mume nimefuga fumbwe! Wewe mwanamume wa aina gani?” alimkabili.

“Mama watoto, kuna shida gani jamani? Mbona vita?” polo aliuliza.

“Nitakacho kujua ni jumbe hizi zatoka kwa kina nani?” mke aliuliza akimwonyesha polo zile arafa.

“Hao ni marafiki zangu tu,” kalameni alijibu baada ya kimya cha muda.

“Kwa hivyo mie ni mjinga!” mama watoto aliwaka kabla kumrukia polo na kumparuza usoni.

Kutokana na kuvuliwa taulo, polo alishindwa kujitetea akiwa uchi.

“Utaniumiza jamani! Mke wangu naomba msamaha, unaniumiza,” jamaa alilia kwani kuna sehemu mama alikuwa amemkamata.

“Nikijua tena una mpenzi, hiyo ‘doshi’ uringayo nayo nitaikata. Wallahi nitaikata!” mke alionya akimwacha na kuondoka.

Siku hizi polo ametulia kama maji ya mtungi wala mademu wakimpigia simu hazipokei.