• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Kocha mbishani Eymael afukuzwa Afrika Kusini

Kocha mbishani Eymael afukuzwa Afrika Kusini

Na JOHN ASHIHUNDU

ALIYEKUWA kocha wa AFC Leopards, Luc Eymael, kuagana kwake na klabu ya Chippa United kulitokana na misukumo ya kisiasa.

Eymael alitimuliwa Jumatano, siku chache baada ya kuteuliwa kama Mshauri Mkuu wa Idara ya Kiufundi ya klabu hiyo ya Afrika Kusini.

“Tumeamua kutoendelea na Eymael, ambaye amekubali kuondoka nchini na kuelekea nyumbani Ubelgiji. Kwa hakika hatungempa kazi iwapo madai yote yaliyowasilishwa yangetufikia mapema,” taarifa ya Chippa United ilisema.

Kutimuliwa kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 61 kulifuatia presha kutoka kwa vyama vya kisasa na makundi ya mashabiki wa soka nchini humu kufuatia kuajiriwa kwake.

Makundi hayo yakiongozwa na lile la Economic Freedom Fighters (EFF) yalikuwa mstari wa mbele kupinga kuajiriwa kwake kutokana na matamshi yake ya hapo awali kuhusu ubaguzi wa rangi.

“Tunapinga vikali kuteuliwa kwa Eymael na tunamtaka mmiliki wa klabu Siviwe Mpengesi abatilishe uamuzi wake wa kumpa kazi Eymael,” kundi la EFF lilisema katika taarifa.

“Tungependa kusisitiza hapa kwamba kamwe hatutamkubalia Eymael kufanya kazi mkoani humu, hatakaribishwa, nafasi yake haipo,” iliongeza taarifa hiyo.

Chippa United ambayo kwa sasa inapigania kubakia ligi kuu ya Afrika Kusini (PSL) ilitoa taarifa kueleza sababu za kutengana na kocha huyo aliyeajiriwa kuchukuwa nafasi ya Dan Malesela, baada ya klabu hiyo kuchapwa 5-1 na Maritzburg United.

Mbali na AFC Leopards na Yanga, Eymael aliwahi kunoa klabu za Rayon Sport nchini Rwanda, El Merreikh (Sudan), Free State Stars (Afrika Kusini) na pia nchini Libya na Oman.

Hii ni mara ya pili kwa Eymael kufukuzwa na klabu baada ya hapo awali kutimuliwa na Yanga kufuatia matamshi yake ya kiubaguzi wa rangi.

Eymael alifukuzwa nchini Tanzania kwa njia isiyoeleka mnamo 2020, alipowafananisha mashabiki wa klabu hiyo na Wanyama wa mwituni.

Aliwataja mashabiki wa Yanga kama watu wasiofahamu chochote kuhusu soka, matamshi ambayo yalisababisha kufutwa kwake. Mbali na kufutwa, Chama cha Soka Tanzania (TFF) kilimpiga marufuku kufanya kazi nchini humo kwa muda usiojulikana.

You can share this post!

KILIMO NA ELIMU: Digrii haikuwa kiunzi kwake kuzamia kilimo...

Liverpool ni muujiza tu sasa UEFA ila Zidane asema kazi...