• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Viongozi wasifu wakazi wa Garissa kwa urithi wa Haji

Viongozi wasifu wakazi wa Garissa kwa urithi wa Haji

Na WACHIRA MWANGI

BARAZA la Maimamu na Wahubiri nchini (CIPK) limepongeza hatua ya wazee katika Kaunti ya Garissa kwa kumteua seneta mpya kupitia kwa demokrasia ya maelewano.

Katibu wa Mipango wa CIPK, Sheikh Mohamed Khalifa, aliwahimiza Wakenya waige mfano huo wa watu wa Garissa katika kumchagua Seneta Abdulkadir Haji baada ya kifo cha baba yake Yusuf Haji mapema mwaka huu.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimuorodhesha rasmi Haji kuwa seneta mteule kumrithi baba yake, baada ya kutojitokeza mtu wa kupingana naye.

Katika arifa kwenye gazeti rasmi la serikali mnamo Jumanne, mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati alithibitisha kufanyika kwa uteuzi kwa kukosekana mpinzani na hivyo kumtawaza Bw Haji kuwa seneta mteule wa Kaunti ya Garissa.

Sheikh Khalifa alisema iwapo taifa hili litaiga mfano huu, basi tume ya uchaguzi itaokoa pesa nyingi za mlipa-ushuru na pia kupunguza siasa zinazotokana na kampeni za uhasama.

“Watu wa Garissa, viongozi wa ukoo, viongozi wa dini na wale wengine walikubaliana wasimamishe mtu mmoja. Hili ni jambo la busara na ni njia moja ya demokrasia. Huu ni mfano mzuri. Kwamba watu wanapokaa na kukubaliana wanaweza kuepusha mambo mengi mabaya.”

Sheikh Khalifa alisema uchaguzi hasa katika mazingira ya sasa, itakuwa vigumu wananchi kuzingatia kanuni za wizara ya Afya kuepuka kusambaa kwa maradhi yavirusi vya corona.

Pia watu wataishia kukoseana heshima kupitia kwa uchochezi na uhasama kati ya makabila na hata dini.

Aliwarai viongozi wengine na Wakenya kwa jumla kuiga mfumo huo katika kuchagua viongozi katika maeneo ambapo wanasiasa wameaga wakiwa mamlakani.

Sheikh Khalifa alisema kwamba Wakenya walitamaushwa na fujo zilizotokana na kampeni maeneo ya Matungu, Kabuchai na katika Kaunti ya Nakuru.

“Tumeona mifano mibaya na hivyo basi hakuna ubaya wowote watu wakikubaliana ili uchaguzi wa pekee uwe ni ule tunaosubiri 2022.

“Viongozi wa maeneo mengine wanafaa wakae chini wasikizane na waelewane. Ikiwa watu wa Garissa wameweza, kwa nini kwingine kusiwe na mfano kama huo?” Sheikh Khalifa aliuliza.

Alisema wakati kura zikipigwa, watu wachache ndio wanaojitokeza kwa sababu ya uoga na hofu ya fujo.

“Kenya kuna shida kubwa ya fedha hivi sasa na tukifuata mfano huo, tutaweza pata matumizi mengine ya fedha zitakazotumika katika hizi uchaguzi mdogo,” Sheikh Khalifa alieleza na kupendekeza kuwa wanasiasa watulize boli za kisiasa, wakubaliane na waepushe wakenya shida zinazokuja na uchaguzi.

You can share this post!

MCK yalaani mauaji katili ya mwanahabari wa KBC

Dawa za kutibu akili taahira zinapogeuzwa ulevi wa mauti