• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
JAMVI: Kizungumkuti cha kuteua ‘Rais’ One Kenya Alliance

JAMVI: Kizungumkuti cha kuteua ‘Rais’ One Kenya Alliance

Na CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa One Kenya Alliance (OKA) unakabiliwa na changamoto kubwa ya kuteua mgombeaji wake wa urais huku ukiendelea kujinadi kote nchini.

Hii ni kwa sababu vigogo wote wanne wanaunda muungano wao wanapania kurithi kiti cha urais, Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Agosti 2022.

Wao ni kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi.

Muungano huu ulipata nguvu mwezi jana baada ya wagombeaji wake kuvuna ushindi katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Matungu (Kakamega), Kabuchai (Bungoma) zilizofanyika Machi 4, na uchaguzi mdogo wa useneta wa Machakos uliofanyika mnamo Machi 18.

Vigogo hao walidai kuwa ushindi wa Bw Oscar Nabulindo wa ANC (Matungu), Bw Majimbo Kalasinga wa Ford Kenya (Kabuchai) na Agnes Kavindu Muthama, wa Wiper katika kaunti ya Machakos, ni ishara ya wao kufaulu kutwaa uongozi wa nchi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Tunajivunia ushindi wetu katika chaguzi ndogo za Matungu, Kabuchai na Machakos. Hii ni dalili kwamba muungano wa One Kenya Alliance utashinda katika uchaguzi mkuu ujao kwani lengo letu ni kuleta mwanzo mpya na kuondoa uvundo katika siasa za nchi,” akasema Bw Musyoka kwenye mahojiano katika runinga moja ya humu nchini wiki jana.

Lakini alipoulizwa nani kati yao wanne atapeperusha bendera ya urais katika muungano huo, kiongozi huyo wa Wiper alidinda kutoa jibu la moja kwa moja.

Akasema hivi: “Ni mapema zaidi kujibu swali hilo wakati huu kwani kibarua kilichoko mbele yetu sasa ni kuuza sera za One Kenya Alliance katika pembe zote nchini. Hata hivyo, nina uhakika kila mmoja wetu yuko tayari kuweka kando masilahi yake kwa ajili ya kufanikisha azma ya kuhakikisha kwamba tunatwaa mamlaka mwaka 2022.”

Naye Bw Mudavadi ambaye mwaka jana alisema kuwa jina lake sharti liwe kwenye karatasi za uchaguzi wa urais, anasema itakuwa rahisi kwa wao kuelewana kuhusu nani kati yao atawania urais kwani “maoni, sera na itikadi yetu ni moja.”

“Ikiwa tulielewana na tukaungana nyuma ya mgombeaji mmoja katika chaguzi ndogo za Matungu, Kabuchai na Machakos, mbona tushindwe kuelewana kuhusu kiti cha urais 2022,?” akauliza kiongozi huyo wa ANC.

Lakini wandani wa vigogo hao wanne tuliozungumza nao kwa ajili ya kuandaa makala hii walitoa mseto wa hisia kuhusu suala hilo la ni nani anafaa kupeperusha bendera ya muungano wa OKA katika uchaguzi mkuu ujao.

Japo anakiri kwamba muungano huo unakabiliwa na kibarua kigumu katika mpango mzima wa uteuzi wa mgombeaji urais, mbunge wa Tiaty William Kamketi (Kanu) anasema kuwa seneta Moi ndiye anafaa kupewa nafasi hiyo.

“Kazi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu vigogo wetu wote wanne wanatosha. Lakini miongoni mwa wote hao ni Gideon pekee ambaye hajawahi kuwania urais na hivyo anafaa kujaribiwa kwa sababu ndiye hajawahi kugombea kiti hicho katika chaguzi zilizopita,” anasema.

Bw Musyoka aliwania urais kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo aliibuka wa tatu nyuma ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais mstaafu Mwai Kibaki. Alipata jumla ya kura 867,045, nyingi za kura hizo zikitoka katika ngome yake ya Ukambani.

Naye Bw Mudavadi aliwania urais kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa 2013 ambapo alipata kura 568,456 kwa tiketi ya chama cha United Democratic Front (UDF). Rais Kenyatta ndiye aliibuka mshindi katika uchaguzi huo akifuatwa na Bw Odinga.

Kwa upande wake, Bw Wetang’ula alijiondoa katika kinyang’anyiro cha urais mnamo 2017 na kuunga mkono Bw Odinga aliyepeperusha bendera ya muungano wa Nasa. Aliahidiwa cheo cha Waziri wa kusimamia watumishi wa umma Nasa ingeshinda na kuunda serikali.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala pia anaungama kuwa muungano wa One Kenya Alliace una kibarua kigumu kuteua mgombeaji wake huku akipendekeza kubuniwa kwa jopo maalum la kuendesha shughuli ya uteuzi wa mpeperushaji bendera ya urais.

“Nakubali ni changamoto kuu wakati huu ikizingatiwa mmoja wa wapinzani wetu kama vile Naibu Rais tayari ameanza kuchapa kampeni za urais. Lakini japo napendekeza kiongozi wangu Bw Mudavadi ndiye apewe tiketi hiyo, ingekuwa bora kama shughuli ya uteuzi ingeendeshwa na jopo maalum lenye wawakilishi kutoka vyama tanzu katika One Kenya Alliance,” akasema Bw Malala.

Seneta huyo wa Kakamega anaongeza kuwa wakati huu ANC iko mbioni kujiimarisha kote nchini kupitia usajili wa wanachama wapya kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wapya kuanzia ndani ya mashinani hadi kitaifa.

“Naamini kwamba baada ya kukamilishwa kwa shughuli hii, ANC kitakuwa thabiti na kupata sura ya kitaifa, hali ambayo itaboresha nafasi ya kiongozi wetu Mudavadi kuteuliwa kuwa mgombeaji urais wa One Kenya Alliance,” akaeleza seneta Malala.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismas Mokua anasema kuwa kigezo kikubwa ambacho kitatumiwa kuamua ni nani miongoni mwa vinara hao wanne wa One Kenya Alliance ni idadi ya kura ambazo kila mmoja wao anaweza kuleta.

“Kwa mfano Mudavadi na Wetang’ula watalazimika kuwashawishi wenzao kwamba moja wao akiteuliwa ataweza kuleta jumla ya kura zaidi ya 3 milioni za uliokuwa mkoa wa magharibi. Eneo hilo linajumuisha kaunti za Kakamega, Bungoma, Vihiga, Busia na sehemu kubwa ya kaunti ya Trans Nzoia. Hii ni kando na kura za watu kutoka jamii ya Waluhya wanaoishi maeneo mengine ya nchi,” anasema.

“Naye Bw Musyoka atahitaji kutoa hakikisho kwamba atavuna jumla ya kura 1.7 milioni za eneo la Ukambani na zingine za kutoka nje ya eneo hili. Lakini Seneta Moi atakuwa na kibarua kigumu kwa sababu sehemu kubwa ya zaidi ya kura 3.5 milioni kutoka Rift Valley ziko mfukoni mwa Dkt Ruto,” anaongeza Bw Mokua.

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba katika mkutano waliofanya Jumapili wiki jana nyumbani kwa Bw Wetang’ula, mtaani Karen, vinara hao wa One Kenya Alliance walipendekeza kubuniwa kwa sekritariati itakayoongoza shughuli zake.

Asasi hiyo pia inatarajiwa kuweka mikakati ya kubuniwa kwa kitengo kitakachosimamia masuala ya teuzi za wagombeaji wa muungano kutoka ngazi ya udiwani hadi urais.

You can share this post!

Bunge halitachelewesha BBI – Muturi

JAMVI: Ni mwanzo mpya katika dunia ya Suluhu, Biden