• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
JAMVI: Ni mwanzo mpya katika dunia ya Suluhu, Biden

JAMVI: Ni mwanzo mpya katika dunia ya Suluhu, Biden

Na WANDERI KAMAU

DUNIA inapitia mapambazuko mapya kisiasa katika ngazi ya kimataifa, kufuatia mageuzi makubwa ya kisera ambayo yameanzishwa na marais wapya Samia Suluhu wa Tanzania na Joe Biden wa Amerika.

Ni mwelekeo mpya wa kisera katika dunia ambayo ilikuwa imezoea mbwembwe, semi kali na misimamo tata ya marais John Magufuli (Tanzania) na mwenzake, Donald Trump (Amerika) hali iliyoathiri sana mahusiano ya nchi hizo na jamii ya kimataifa.

Nchini Tanzania, Rais Suluhu tayari ameanza kuondoa baadhi ya sera tata alizoendeleza Dkt Magufuli, hali inayotajwa kuanza kugeuza mwelekeo wa taifa hilo katika ulingo wa kimataifa.

Kwa muda wa wiki mbili tu, kiongozi huyo ameagiza kutathminiwa upya kwa msimamo wa Tanzania kuhusu janga la virusi vya corona, kuondolewa kwa marufuku iliyokuwa imewekewa baadhi ya vyombo vya habari na kuwaagiza maafisa wa serikali yake kutotumia nguvu wanapowatoza kodi wawekezaji kutoka nje.

Akilihutubia taifa hilo Jumanne baada ya kuwaapisha makatibu wapya wa kudumu wa wizara na wakuu wa idara mbalimbali za serikali, Bi Suluhu alisema Tanzania inahitaji kuwa na msimamo unaobainika kuhusu janga la corona.

“Hatuwezi kujitenga kama sisi ni kisiwa. Hatuwezi kukubali chochote tutakacholetewa, lakini hatuwezi kuendelea kusoma takwimu kuhusu maambukizi ya corona duniani ilhali hali yetu haijulikani,” akasema Bi Suluhu.

Tanzania ilitoa maelezo yake ya mwisho kuhusu corona Aprili 2020 na haijawahi kutoa maelezo mengine baada ya Dkt Magufuli kutangaza kwamba “imelishinda janga hilo.”

Kutokana na mwelekeo huo mpya, wadadisi wanasema kuwa huenda uongozi wa Rais Suluhu ukaashiria mwanzo mpya kwa sura ya Tanzania katika ulingo wa kimataifa, baada ya uongozi wa Rais Magufuli kuonekana kuitenga, hasa na majirani wake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama Kenya, Uganda, Burundi, Sudan Kusini na Rwanda.

“Mwelekeo ambao Rais Suluhu ameanza kuonyesha unaashiria kama mwanzo wa safari ya kuondoa makosa ambayo Dkt Magufuli alifanya. Ingawa bado ni mapema, huenda lengo lake kuu ni kurejesha uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na nchi zingine,” asema Dkt Godfrey Musila, ambaye ni mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa.

Katika kujaribu kurejesha uhuru wa vyombo vya habari, wadadisi wanasema Bi Suluhu analenga kurejesha urafiki wa Tanzania na nchi kama Amerika na Uingereza, ambazo zilikuwa zikimkosoa sana Dkt Magufuli kwa sera zake kali dhidi ya vyombo hivyo.

Chini ya utawala wa Magufuli, serikali ya Tanzania ilifunga magazeti mengi yaliyochapishwa kwa njia ya mtandao, na yaliyoandika habari ama makala ya kukosoa serikali yake.

Baadhi ya magazeti yaliyofungwa ama kupigwa faini kwa kumkosoa kiongozi huyo ni The Citizen, Mwananchi, Mawio, Mwanahalisi kati ya mengine.

Wanahabari pia walijipata pabaya, baadhi yao wakitoweka katika hali tatanishi. Miongoni mwa wanahabari hao ni Azory Gwanda, ambaye alitoweka katika hali tatanishi mnamo 2017, huku mwenzake, Erick Kabendera akikamatwa na kuzuiliwa korokoroni kwa tuhuma za kuandika habari za “kichochezi.” Katika ulingo wa kisiasa, uhusiano wa Tanzania na majirani wake uliathirika sana, kiasi kwamba marais wa nchi za EAC walikwepa kuhudhuria mazishi ya Dkt Magufuli, kando na Rais Uhuru Kenyatta.

Kulingana na Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa za kimataifa, uhuru wa vyombo vya habari ni miongoni mwa vigezo ambavyo nchi nyingi za Magharibi huangalia katika kuendeleza urafiki wake na mataifa ya Afrika.

“Nchi kama Uingereza na Amerika hutilia maanani sana uzingatiaji wa masuala ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu. Hiyo ndiyo sababu ambapo Rais Suluhu ameanza kutathmini upya baadhi ya misimamo iliyoendeshwa Dkt Magufuli ili kurejesha urafiki kati ya Tanzania na mataifa hayo,” akasema Bw Muga.

Rais Suluhu pia ameagiza idara za serikali kutowahangaisha wawekezaji kutoka nchi za nje, akiwataja kama mhimili mkuu katika ukuzaji wa uchumi wa taifa hilo. Chini ya mwamko huo mpya, wadadisi wanaeleza dunia itashuhudia mwelekeo mpya katika masuala ya kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi, kwani hata Rais Biden wa Amerika ameanza kuondoa baadhi ya sera tata zilizoendeshwa Trump.

Miongoni mwa sera hizo ni kurejesha uhusiano na baadhi ya mataifa ambayo Trump alikuwa amepiga marufuku raia wake kwenda Amerika kwa kisingizio cha kuendesha ugaidi.

Hatua hiyo iliathiri sana urafiki wa Amerika na Afrika, hasa baada ya nchi kama Sudan na Somalia kujipata kwenye orodha hiyo tata.

Kijumla, wadadisi wanaeleza kuwa kuondoka kwa marais Trump na Magufuli kutaathiri sana mahusiano na sera za kimataifa za nchi hizo, kwani wawili hao waliziongoza kama kwamba “haziwezi kuyategemea mataifa yale mengine.”

“Misimamo mikali ya viongozi hao haikuathiri tu nchi zao katika ngazi ya kimataifa, bali mahusiano kati ya raia katika mataifa jirani. Kuondoka kwao ni funzo kubwa kwamba kwa taifa kustawi katika nyanja zote, linahitaji kushirikiana na nchi zingine,” asema Dkt Amukowa Anangwe, ambaye ni msomi na mchanganuzi wa masuala ya kimataifa.

Kulingana naye, kuna uwezekano mkubwa mikakati ya kufufua upya EAC kuanza kushika kasi, kwani Rais Suluhu ameonyesha nia ya kuziba pengo lililokuwepo kwenye mahusiano ya taifa lake na wanachama wa EAC.

You can share this post!

JAMVI: Kizungumkuti cha kuteua ‘Rais’ One Kenya Alliance

JAMVI: Kukwama kwa refarenda Juni kutakavyomjenga Ruto