• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
JAMVI: Kukwama kwa refarenda Juni kutakavyomjenga Ruto

JAMVI: Kukwama kwa refarenda Juni kutakavyomjenga Ruto

Na BENSON MATHEKA

IWAPO kura ya maamuzi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) haitafanyika jinsi ilivyopangwa, Naibu Rais William Ruto atakuwa ameshinda pakubwa na kupata nguvu zaidi kisiasa dhidi ya viongozi wengine wanaounga mchakato huo.

Dkt Ruto hajawahi kuuchangamkia mchakato huo akisema handisheki iliyozaa BBI kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, ililenga kumzuia asigombee urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na kubuni nyadhifa za uongozi kwa watu wachache badala ya kujali maslahi ya wananchi wa kawaida.

Kulingana naye, iwapo ni lazima kura hiyo ifanyike, inafaa kuwa pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022. Amekuwa akisema hakuna dharura ya kubadilisha katiba wakati ambao kuna masuala muhimu ya kushughulikia nchini likiwemo janga na corona na Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee.

Kwa sababu ya kupinga mchakato huo, Dkt Ruto alitengwa serikalini na katika chama tawala cha Jubilee na mapema Februari mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta alimtaka ajiuzulu badala ya kupinga mipango ya serikali.

Bw Odinga amekuwa msitari wa mbele kumshambulia Dkt Ruto kwa kupinga BBI na kura ya maamuzi.

Mipango ya Bw Odinga, ilikuwa ni kura ya maamuzi kufanyika Juni mwaka huu. Mswada wa kura ya maamuzi uliopitishwa na mabunge zaidi ya 40 pia uliweka muda wa mwaka mmoja kutekeleza mabadiliko ya kikatiba na kiusimamizi kupitia BBI.

Wadadisi wanasema kuna kila dalili kwamba huenda kura ya maamuzi isifanyike Juni mwaka huu ilivyopangwa baada ya bunge kusitisha vikao vyake hadi Mei 4, kufuatia maambukizi ya corona.

Kufikia wakati wa kuandika makala haya, hakukuwa na dalili kwamba bunge litaitwa kwa kikao maalumu kushughulikia mswada huo.

Mnamo Alhamisi Spika wa bunge Justin Muturi alisema hakuwa amepokea mawasiliano yoyote yanayoweza kumfanya kuita kikao spesheli cha bunge kujadili mswada wa kura ya maamuzi wa BBI.

“Kamati ( ya pamoja ya bunge na seneti) hazijawasilishwa ripoti yake na bila ripoti hiyo kikao spesheli cha bunge hakiwezi kuitwa kwa kuwa hakutakuwa na cha kujadili,” akasema Muturi.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kutofanyika au kukwama kwa refarenda kutakuwa ushindi mkubwa kwa Dkt Ruto, sio kwa sababu amekuwa akipinga mchakato huo, bali kuwa amekuwa akijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022 wakati wanasiasa wengine wanaomezea mate urais walikuwa wakiuunga mkono.

Kutoaminiana

“Japo alionekana pekee akipinga mchakato huo huku wanasiasa wengine wakuu wakiuunga mkono, kutofanyika kwa kura ya maamuzi kutamfaa zaidi. Kumbuka amekuwa akisema kuna masuala muhimu yanayofaa kushughulikiwa badala ya kura ya maamuzi,” asema mchanganuzi wa siasa David Wafula.

Anaeleza kuwa kumetokea dalili za kutoaminiana kati ya kambi za Rais Kenyatta na Bw Odinga kunakoweza kusambaratisha mpango mzima wa kubadilisha katiba kwa manufaa ya Dkt Ruto ambaye atatumia kufeli kwa kura ya maamuzi kujipigia debe kwenye kampeni za uchaguzi mkuu ujao.

Wadadisi wanasema kura ya maamuzi inaweza kufanyika tu kabla ya Agosti mwaka huu au pamoja na uchaguzi mkuu ujao.

“Ikiwa itafanyika pamoja na uchaguzi mkuu ujao, Dkt Ruto pia atakuwa ameshinda kwa kuwa amekuwa akipendekeza hilo. Kwa vyovyote vile, kutofanyika kwa kura ya maamuzi, au ikifanyika pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022, iwapo hilo linawezekana,

itakuwa baraka kwa Dkt Ruto na pigo kubwa kwa waasisi, wanamikakati, wanaounga na wanaotegemea mchakato huo kuondoka katika baridi ya kisiasa,” asema mchanganuzi wa siasa Peter Katana Kalume.

“Je, waasisi na watetezi wataambia nini Wakenya kura ya maamuzi ikikosa kufanyika ilhali Dkt Ruto aliipinga na wakampuuza wakimuita kila aina ya majina hadi akatengwa serikalini?” asema Katana.

“Wakisingizia janga la corona, itakuwa ni kukubaliana na Dkt Ruto ambaye amekuwa akisisitiza kwamba BBI haifai kupatiwa kipaumbele wakati wa janga hilo. Watakuwa wamemjenga huku wakiaibika,” asema.

Wadadisi pia wanasema kusambaratika kwa mchakato huo kutamfaidi Dkt Ruto huku dalili zikionyesha huenda akaungana na Bw Odinga baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kuhisi kwamba Rais Kenyatta hana nia ya kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wachanganuzi wanasema iwapo Dkt Ruto na Bw Odinga wataungana, ni naibu rais atakayenufaika pakubwa ikizingatiwa amekuwa akipigwa vita na mkubwa wake Rais Kenyatta ambaye duru zinasema anampendelea Seneta wa Baringo Gideon Moi, hasimu mkuu wa Dkt Ruto katika eneo la Rift Valley.

Bw Moi ni kiongozi wa chama cha Kanu ambacho kimeungana na Wiper cha Kalonzo Musyoka, Amani National Congress cha Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha Moses Wetangula kuunda muungano wa One Kenya Alliance unaosemekana kuwa na baraka za Rais Kenyatta.

Wadadisi wanazidi kuhoji kwamba wanne hao wanategemea nyadhifa zilizopendekezwa kwenye mswada wa kubadilisha katiba wa BBI.

Ni muungano huu ambao wachanganuzi wanasema umechangia uhusiano baridi kati ya waasisi wa mchakato wa kubadilisha katiba huku chama cha ODM kikihisi kwamba Bw Odinga anachezwa na hivyo kumfanya kutafuta Dkt Ruto waungane kisiasa.

You can share this post!

JAMVI: Ni mwanzo mpya katika dunia ya Suluhu, Biden

JAMVI: Mjane atakuwa mbunge wa kike wa kwanza Kisii?