• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
JAMVI: Mjane atakuwa mbunge wa kike wa kwanza Kisii?

JAMVI: Mjane atakuwa mbunge wa kike wa kwanza Kisii?

Na WYCLIFFE NYABERI

MEI 18, wakazi wa eneobunge la Bonchari, Kaunti ya Kisii watakwenda debeni kumchagua mbunge wao mpya baada ya kifo cha Oroo Oyioka aliyeaga dunia mwezi Februari kutokana na maradhi ya kisukari.

Kwenye uchaguzi huo mdogo, wanawake watatu watajimwaya debeni kumenyana na wanaume kumi katika kinyang’anyiro ambacho wengi wametabiri kitakuwa kivumbi kikuu.

Wawaniaji hao wanawake ni Bi Teresa Bitutu ambaye ni mjane wa marehemu Oroo Oyioka, atakayepeperusha bendera ya chama kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA), mwakilishi wa kike wa zamani wa kaunti ya Kisii Bi Mary Sally Otara (United Green Movement) na Bi Margaret Nyabuto wa chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC).

Katika jamii ya Abagusii, kama ilivyo katika jamii nyingi nchini, wanawake hawapati nafasi nzuri kuchaguliwa kwenye nyadhifa za uongozi ikilinganishwa na wenzao wa kiume.

Hivyo basi uchaguzi wa Bonchari kwa mara nyingine utaiweka jamii hiyo kwenye mizani ikiwa itakwenda kinyume na mila na itikadi zilizopitwa na wakati na kumpa nafasi mwanamke fursa ya kuongoza au la.

Tangu taifa la Kenya lijinyakulie uhuru na viongozi kuanza kuchaguliwa kwenye nyadhifa mbali mbali za kisiasa, hakuna hata mwanamke mmoja kutoka jamii hiyo amewahi kuchaguliwa kwenye kiti kikubwa cha kisiasa. Wanawake wamekuwa wakijiliwaza tu kwenye viti walivyotengewa na katiba ya 2010.

Ikiwa wanawake watabahatika, basi viti watakavyochaguliwa ni vile vya chini vya uwakilishi Wadi. Kwa mfano, ni wanawake wawili tu waliopata nafasi ya kuchaguliwa kama madiwani katika mabunge ya sasa ya kaunti za Kisii na Nyamira. Wao ni Bi Rosa Kemunto wa Majoge Bassi na Bi Callen Atuya wa Bokeira.

Japo wawaniaji hao wanawake wameonyesha imani kuwa watazivunja taasubi za kiume na hulka za wanawake kutochaguliwa na kuandikisha historia ya mmoja wao kuibuka mshindi kwa mara ya kwanza, bado kibarua ni kigumu ikizingatiwa wanawake hao watalazimika kuwakabili wawaniaji wengine waliopewa tikiti na vyama vikuu nchini kama vile Jubilee na ODM.

Jamvi lilitafuta maoni ya wachanganuzi wa siasa na wazee kutoka jamii ya Abagusii ili kutathmini ni kwa nini wanawake hupata wakati mgumu kuuza sera zao kwa wapigakura wanapotafuta kuchaguliwa.

Kulingana na katibu wa Baraza la wazee wa jamii ya Abagusii Bw Samuel Bosire, wanawake wachache jasiri wanaojitokeza kuwania viti vya kisiasa hukumbana na mazingira ya kisiasa ambayo yamejaa uhasama, kejeli na matusi kutoka kwa wapigakura ambao huwadharau wanawake na kuwaona kuwa hawafai kuwania uongozi.

Badala yake, Mzee Bosire anadokeza kuwa wapiga kura hasa wanaume huwaona kina mama kama walioharibika wanaposimama kupingana na wanaume kisiasa.

Hata hivyo, katibu huyo alisema kuwa kina mama huibuka kuwa viongozi wazuri na hivyo basi jamii inafaa kuwajaribu kwenye kazi hizo.

Alitolea mfano Rais wa Muungano wa Jamhuri ya Tanzania Bi Suluhu Hassan na kusema huu ni wakati wa jamii za Kenya kuwaamini wanawake katika nyadhifa za uongozi kwani wengi wameonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza vyema.

Bi Rachael Otundo, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa machache ya Afrika ambayo yameweka mikakati ya kuimarisha uongozi kwa kubuni vitengo mbali mbali vya utawala lakini bado mengi yanafaa kufanywa ili kuziba mwanya wa kijinsia unaoshuhudiwa kwenye siasa. Hivyo basi, Bi Otundo anashikilia kuwa uamuzi wa vyama vya UDA, UGM na MCC kuwapa wanawake tikiti ya kujaribu bahati zao Bonchari kumrithi marehemu Oyioka ni nzuri na inayofaa kuungwa mkono.

Bi Bitutu katika kampeni zake amekuwa akiwarai wakazi wampe nafasi akamilishe kipindi cha mumewe na anashikilia kuwa ni yeye anayeifahamu vyema kazi aliyokuwa ameanzisha mumewe.

Naye Bi otara anasema kuwa alipokuwa mwakilishi wa kike, kuna mengi aliyoyafanikisha na angependa kuendeleza miradi aliyoachia njiani ikiwemo ya kuwapa sauti watu wasiojiweza na walemavu. Bi Nyabuto naye amejinadi kuwa msomi na anayejua shida za watu waishio vijijini. Amedokeza kuwa akipewa nafasi, ataimarisha viwango vya elimu Bonchari lakini uamuzi wa mwisho ni wa mpiga kura.

Wanawake hao watakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Bw Zebedeo Opore (Jubilee), Mhandisi Pavel Oimeke (ODM), Jonah Onkendi (The New Democrats) Kelvin Mosomi (Party of Democracy Unity), Mokaya Charles (Progressive Party of Kenya), Atancha Jeremiah (Agano Party), Matagaro Paul (Mwangaza Tu), Victor Omanwa (Party of Economic Democracy), David Ogega (Kenya Social Congress) na Eric Oigo (National Reconstruction Alliance).

You can share this post!

JAMVI: Kukwama kwa refarenda Juni kutakavyomjenga Ruto

Uingereza yapongezwa kwa kuwa na msimamo chanya kuhusu...