Raila awindwa na Uhuru, Ruto

JUSTUS WANGA na WANDERI KAMAU

UKURUBA wa kisiasa unaoendelea kudhihirika kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, umeibua wasiwasi miongoni mwa washirika wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hali hiyo imewachochea kuandaa msururu wa mikutano, baadhi yao iliyohudhuriwa na Rais Kenyatta.

Jumamosi, Rais Kenyatta alitarajiwa kukutana na Bw Odinga kufuatia mkutano uliofanyika Jumatano kati ya Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega na Dkt Ruto katika eneo la Maasai Mara, Kaunti ya Narok.

Mkutano huo ulipangwa “kujadili kuhusu hali ya handisheki kutokana na mwelekeo mpya wa kisiasa nchini.”

“Nilisikia kuhusu mkutano huo ingawa sijui kama ulifanyika,” akasema Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe, kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.

Mbunge ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Odinga alisema mkutano huo ulipangiwa kufanyika ama jana Jumamosi au leo Jumapili.

“Huenda wasitoe picha kwa umma kama mlivyoona wengine wakifanya. Ni kweli kuna mkutano uliopangiwa kufanyika wikendi hii,” akasema, akiongeza kuna haja kuzihakikishia kambi za kisiasa za viongozi hao wawili kwamba kila kitu ki shwari.

Wandani wa karibu wa Rais Kenyatta wanasema kwa kubuni ushirikiano na Dkt Ruto, Bw Odinga atakuwa amempotezea Rais miaka mitatu, hasa kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), hatua ambayo pia ilimfanya kukosana kisiasa na Dkt Ruto.

“Bw Oparanya anatuambia ulikuwa tu mkutano wa kawaida. Kwingineko anasema Bw Odinga alifahamu kuhusu uwepo wake. Tutangoja kusikia moja kwa moja kutoka kwa Bw Odinga,” akasema Bw Murathe, ambaye ni mshirika wa Rais Kanyatta.

Ilibainika mwelekeo huo umezua wasiwasi katika kambi ya kisiasa ya Rais Kenyatta, washauri wake wakihofu kwamba itawalazimu kuanza mikakati mipya kisiasa ikiwa watawapoteza Bw Odinga na Dkt Ruto kwa wakati mmoja.

Kufuatia hayo, wadadisi wa siasa wanasema nia ya Bw Odinga ni kudhihirisha kuwa bado ni mwanasiasa mwenye maono, na hawezi kukosa kufanya maamuzi mbadala ikiwa atasalitiwa.

Tangu 2018, Bw Odinga amekuwa kwenye ushirikiano wa kisiasa na Rais Kenyatta, maarufu kama handisheki.

Hata hivyo, ushirikiano huo umeonyesha dalili za kuyumba, baada ya ripoti kuibuka kwamba Rais Kenyatta anaupendelea muungano wa kisiasa wa One Kenya Alliance.

Muungano huo unawashirikisha kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na mwenzake Gideon Moi (Baringo).

“Lengo la Bw Odinga ni kuonyesha kuwa bado ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa kisiasa nchini. Analenga kuwaonyesha washindani wake kuwa ana njia mbadala za kujijenga ikiwa wataendesha njama zozote kujaribu kumzima kisiasa,” akasema Bw Mark Bichachi, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Vile vile, wadadisi wanasema kuwa lengo lingine ni kuwadhihirishia Wakenya, Rais Kenyattta na washindani wake kisiasa kwamba, hata yeye anaweza kufanya maamuzi ambayo yanaweza kuutikisa ulingo wa kisiasa nchini.

“Baada ya Rais Kenyatta kudaiwa kuunga mkono muungano wa One Kenya Alliance, ilimdhihirikia Bw Odinga na ODM kuwa si lazima rais amuunge mkono moja kwa moja kuwania urais 2022. Hivyo, imembidi Bw Odinga kudhihirisha pia yeye ni mwanasiasa anayeweza kuvuruga na kusambaratisha njama za kisiasa anazopanga Rais Kenyatta na waandani wake,” akasema mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo.

Wadadisi wanasema huenda isiwe vigumu kwa wawili hao kushirikiana, kwani wote watafaidika kwa kufanikiwa kuvuruga mikakati ya kisiasa ya Rais Kenyatta na muungano wa One Kenya Alliance.

Mnamo 2007, wawili hao walihudumu katika baraza la ‘Pentagon’ wakati Bw Odinga aliwania urais kwa tiketi ya ODM.

Hata hivyo, walikuwa kwenye kambi tofauti kisiasa kwenye kura ya maamuzi 2010 kuhusu Katiba ya sasa.

Habari zinazohusiana na hii

Wapuuza Uhuru

Raila amezea mate OKA