• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
MKU kwenye mstari wa mbele katika masuala ya michezo

MKU kwenye mstari wa mbele katika masuala ya michezo

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) hivi majuzi kilijiunga na ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Michezo kwa ajili ya Amani na Maendeleo katika Eneo la Afrika.

Mkutano huo ulioendeshwa kupitia mtandao ulishirikisha MKU na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Elimu Sayansi na utamaduni (Unesco) kwa minajili ya mafunzo ya kujiendeleza kimaendeleo.

Wengine walioshiriki ni chama cha michezo bara Afrika – The Africa Sports Association – na kituo cha habari cha TV 47.

Mwongozo halisi wa mipango hiyo ulikuwa kuinua michezo kwa kujihusisha na mazoezi ya mara kwa mara ili kuwa katika afya njema.

“Tunaweza kuzuia maradhi mengi kuingia miilini mwetu iwapo tutazingatia mazoezi ya kila mara hasa mbio,” alinukuliwa Eliud Kipchoge wakati mmoja alipokamilisha mbio za marathon chini ya saa 1.59, mwaka wa 2019.

Baada ya miaka miwili maneno yake yanaonekana kupata uzito wake kwa sababu siku hizi watu wengi wamerejelea mazoezi.

Maradhi ya Covid-19 yanafanya michezo kuchukua nafasi muhimu katika maisha ya binadamu kwa sababu mazoezi yanasaidia kulinda mtu kuwa sawa; kiakili na kimwili.

Mkurugenzi wa shirika la Unesco Irina Bokova, wakati mmoja alipendekeza watu wafanye mazoezi kwa ushirikiano kwa lengo la kuwa katika hali njema ya kiafya.

“Tunawahimiza Wakenya na watu wengine popote walipo wazingatie kuzamia katika mazoezi ya kimwili ili kuepukana na maradhi mengi yanayotuzingira mwilini ikiwemo covid-19,” alisema Dkt Vincent Gaitho ambaye ana cheo kinachokaribia kile cha naibu chansela ambacho kitaaluma kinafahamika kama pro-chancellor MKU.

Alisema homa ya Covid-19 imevuruga mambo mengi katika ulimwengu wote kwa ujumla na kwa hivyo “ni muhimu kila mmoja kujichunga ili ajiepushe na janga hilo.”

“Janga hilo limeathiri mambo mengi ulimwenguni kote ambapo mengi mazuri yaliyokuwepo yamezama huku kila mmoja akija na mbinu tofauti ya kujiendeleza kimaisha,” alifafanua Dkt Gaitho.

Alitoa wito kwa Wakenya kufuata masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya ili “tuweze kukabiliana na janga hilo”.

Alisema kila mmoja popote alipo ana jukumu la kuona ya kwamba anajikinga dhidi ya homa hiyo bila kungoja serikali kufuatilia.

You can share this post!

Omar alitumia ‘juju’ kuzubaisha mpenziwe, korti...

Chitembwe alilia kazi ya Maraga akihojiwa