• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 AM
Hofu msitu kugeuka uwanja wa mauti

Hofu msitu kugeuka uwanja wa mauti

CORNELIUS MUTISYA Na CHARLES WASONGA

MSITU wa Iveti, ulioko katika kaunti ya Machakos unasifika kwa mandhari ya kuvutia yanayotokana na aina mbalimbali ya miti na mimea mingineyo inayousuka. Ni chemchemi kuu ya maji katika kaunti hii na maeneo ya karibu.

Mingi ya miti katika msitu huu, unaounganisha eneobunge la Kathiani na lile la Machakos Mjini, ni ya kiasili iliyopandwa katika enzi wa ukoloni. Ni rasilimali muhimu ya kitaifa iliyoko chini ya usimamizi wa Shirika la Misitu Nchini (KFS).

Hata hivyo, sifa nzuri ya msitu huu inatiwa doa na visa vya mauaji vinavyotekelezwa ndani yake na kuwatia wakazi wa maeneo haya wengi hofu na jitimai.

Visa hivyo, ni kielelezo cha utovu wa usalama katika maeneo yaliyoko karibu na msitu huo wa Iveti.Mwezi uliopita, mwanamume wa umri wa makamo alipatikana ameuawa kinyama kwa kukatakatwa na mwili wake kutupwa ndani ya msitu huu wenye ukubwa wa zaidi ya hekta 62.

Wapita njia waliupata mwili huo kando ya kijia kimoja kinachopitia katikati ya msitu huo, hatua chache karibu na soko Kaviani, mwendo wa saa mbili za asubuhi. Walimpasha habari chifu wa Kata ya Iveti Charles Loki ambaye aliwaita maafisa wa polisi kutoka kituo cha Kathiani.

Maafisa hao waliuondoa mwili huo na kuupeleka katika mochari ya Hospitali ya Machakos Level 5 kisha uchunguzi ukaanzishwa.

“Marehemu alikuwa amekatakatwa vibaya sana kichwani na macho yake kudonolewa ishara kwamba huenda aliuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kutupwa kwenye msitu huo ili kupoteza ushahidi,’’ akasema chifu Loki.

Kisa hicho kilitokea mnamo Machi 18 mwaka huu.Afisa huyo wa utawala aliwaambia wanahabari kuwa hicho kilikuwa ni kisa cha tano, mwaka huu, cha mtu aliyeuawa na mwili wake kutupwa ndani ya msitu huo wa Iveti.

“Mwezi mmoja haupiti bila afisi yangu kupata ripoti ya maiti ya mtu kupatikana imetupwa ndani ya msitu huo ambao umegeuka kiwanja cha mauti. Hiki ni kisa cha tano tangu Januari mwaka huu,” akaeleza.

Bw Loki pia alitaja kisa cha mnamo Februari 16, 2021 ambapo mama mmoja alipatikana ameuawa kikatili na mwili wake kuanikwa mtini, akiwa uchi wa mnyama.

Mama huyo (ambaye tunalibana jina lake) alikuwa mkazi wa kijiji cha Kaewa, eneobunge la Kathiani.Licha ya polisi kuchunguza kisa hicho, hakuna mshukiwa yeyote amenaswa kuhusiana na mauaji hayo tatanishi zaidi ya mwezi mmoja baadaye.

Isitoshe, mwaka huu na mwaka jana, kuliripotiwa visa ambapo baadhi ya wafanyabiashara kutoka maeneobunge ya Machakos na Kathiani waliripotiwa kuporwa na kupigwa hadi kufa na miili yao kutupwa katika sehemu tofauti za msitu huu wa mauti.

Kamanda wa Polisi kaunti ya Machakos Moses Nthiwa, alithibitisha habari za visa vya miili ya watu waliouawa kupatikana katika msitu huo wa Iveti huku akiahidi kuwa maafisa wake wameimarisha doria eneo hilo kwa lengo la kuwanasa wahalifu hao.“Afisi yangu imepata habari kuhusu visa hivyo vya mauaji ya kikatili na ya kutatanisha.

Hii ndio maana sasa tumeunga kikosi maalum cha maafisa ambao watakuwa wakishika doria usiku na mchana ndani na nje ya msitu huo. Naamini kuwa tutawakamata hawa makachinja wanaowahangaisha raia wasio na hatia,” akasema.

Bw Nthiwa aliwarai wakazi wawe watulivu na kushirikiana na polisi katika jitihada za kuwawinda wahalifu hao, akisema hiyo ndio njia ya kipekee ya kuzima kero hilo.

“Udumishaji wa usalama sio wajibu wa polisi pekee; mchango wa wananchi ni muhimu zaidi. Wajibu wao ni kutoa habari zitakazotuwezesha kuwatia mbaroni wahuni hao. Hii ndio maana serikali inatekeleza sera mahsusi ya kushirikisha wananchi katika masuala ya usalama,” akaeleza.

Joseph Mutiso ambaye ni mkazi wa kata ya Ngelani, ameitaka serikali ya kitaifa na ile ya kaunti ya Machakos kutekeleza mpango wa pamoja utakaozuia msitu wa Iveti kugeuzwa kuwa mahala pa kufanikisha mauaji.

“Doria ya polisi na maafisa wa misitu haitatosha. KFS kwa ushirikiano na serikali ya kaunti inaweza kutekeleza miradi mbalimbali ya ukuzaji na uboresha wa msitu huu. Tunataka faida sio hasara ya watu kushambuliwa kila mara na kutupwa huko,” anasema.

Mkuu wa Idara ya Misitu kaunti ya Machakos Mary Mwai, alisema mpango wa kugeuza sehemu kubwa ya msitu huo kuwa kivutio cha watalii ni mojawapo na njia za kutekeleza mapendekeza yanayotolewa na watu kama Bw Mutiso.

“KFS kwa ushirikiana na muungano wa wanajamii wanaolinda misitu (CFA) imeanzisha mpango wa Eco-Tourism unaolenga kuboresha msitu huu na kuufanya kivutia cha watalii. Tayari shughuli hiyo inaendelea katika eneo la Rita,” akasema Bi Mwai.

Akithibitisha kauli ya afisa huyo wa KFS, mwenyekiti wa CFA Daniel Musila Kimondiu alisema wameanza kwa kuendesha shughuli za upanzi wa nyasi ya kisasa na maua katika sehemu kadha za msitu huo ili kuuboresha.

“Hatutaki msitu kama huu ambao ni rasilimali muhimu kugeuzwa na wahalifu kama mahala pa kutupa maiti za watu. Huu mradi wa ‘Eco-Tourism’ utauwezesha msitu huu kuwa kivutio kwa watalii wa humu nchini na wale kutoka mataifa ya kigeni. Sote tutafaidi kwayo kwa kuanzisha biashara mbalimbali kama zile za kuuza vinyago,” akaeleza.

You can share this post!

MARY WANGARI: Udangayifu katika mitihani ni tishio kwa...

Knec kuanza kusahihisha KCSE wiki hii