• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Vyoo vya soko la Witeithie vyabomolewa

Vyoo vya soko la Witeithie vyabomolewa

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Witeithie, Juja, Kaunti ya Kiambu, wameshangaa Jumanne asubuhi, wakati vyoo vyao walivyojengewa majuzi kubomolewa na watu wasiojulikana.

Vyoo hivyo kumi vilijengwa ndani ya soko katika eneo hilo na vilitarajiwa kuanza kutumika mwishoni mwa wiki hii.

Mkazi mmoja wa kijiji hicho, Bw Michael Kamau, alisema kitendo hicho ni cha kinyama kwa sababu wakazi wengi watakosa mahali pa kwenda haja na hiyo ni hatari kwa afya ya binadamu.

Kulingana na wakazi wa hapo inadaiwa mwaniaji mmoja wa kiti cha ubunge cha Juja ndiye aliyejitolea kujenga vyoo hivyo huku ikidaiwa mahasimu wake ndio huenda pengine wanalemaza juhudi zake za kuendesha mradi huo.

Mkazi huyo anazidi kudai kuwa baada ya kitendo hicho kushuhudiwa, wachuuzi wa vyakula watakuwa na kibarua kigumu kupata mahali pema pa kujisaidia ama haja ndogo au haja kubwa.

Alisema soko hilo huwa na wachuuzi wa chakula wapatao 1500 kwa wakati moja na kwa hivyo wangetaka hatua ya dharura ichukuliwe haraka iwezekanavyo kabla ya mambo kuharibika.

Naye Bw Joseph Mwangi mkazi wa kijiji hicho alisema wameachwa na mshangao kwa sababu hawajui sasa watafanya lipi, kwani walitarajia kunufaika na vyoo hivyo.

“Sisi kama wakazi wa hapa Witeithie tumekasirika sana kwa sababu jambo tuliyoshuhudia ni la kinyama ambapo watu waliofanya uovu huo wanastahili kuchukuliwa hatua kali na kushtakiwa bila huruma,” alisema Bw Mwangi.

Biashara ilisimama kwa muda wa masaa manne katika kijiji hicho hasa sokoni wakazi hao wakitafakari ni lipi watafanya kutokana na kisanga hicho.

Afisa mkuu wa polisi katika eneo la Juja Dorothy Migarusha alisema tayari amepokea habari hiyo na uchunguzi unaendelea kufanywa ili kubainisha hasa wale waliohusika.

“Tayari maafisa wa upelelezi wanaendelea kufanya uchunguzi ili kujua ukweli wa mambo,” alisema Bi Mogarusha.

Alieleza kuwa kitendo hicho kinatia hofu kwa sababu kinaweza kusababisha watu kuambukizwa maradhi mabaya kwa kukosa choo.

You can share this post!

MAPISHI: Kuku kienyeji

Nyoro ajadiliana na madiwani jinsi ya kufufua miradi...