• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Mfungo wa Ramadhan bila sherehe kwa mwaka wa pili

Mfungo wa Ramadhan bila sherehe kwa mwaka wa pili

NA AP

WAISLAMU kote ulimwenguni walianza kuadhimisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan huku maadhimisho hayo yakigubikwa na visa vya maambukizi ya virusi vya corona, huku sherehe zikipigwa marufuku.

Bara Uropa, ambalo ndilo limeathirika zaidi, lilivuka kiwango cha vifo milioni moja kutokana na Covid-19, huku mataifa ya Asia Kusini yakikabiliana na makali ya ugonjwa huo ambao umelemaza mifumo ya uchumi duniani.

Shughuli za utoaji chanjo zimewapa matumaini watu ambao wamechoshwa na masharti makali ambayo yameingia mwaka wa pili sasa.

India, ambayo inashuhudia kuongezeka kwa visa vya mkurupuko huo, ilipigwa jeki pakubwa kufuatia hatua yake ya kuidhinisha chanjo ya Urusi ya Sputnik V, dhidi ya Covid-19.

Idadi ya jumla ya vifo kutokana na virusi hivyo inaelekea kufika milioni tatu kulingana na takwimu mpya rasmi.

Shirika la Afya Duniani limeonya kuwa, maambukizi yanaongezeka kwa kasi licha ya juhudi za kuyazuia.

Idadi kubwa ya Waislamu kote ulimwenguni, kuanzia Indonesia hadi Misri. walianza Ramadan baada ya viongozi wa kidini kuthibitisha kuwa mwezi wa mfungo ungeanza jana, ingawa masharti kwa waumini yalitofautiana kutoka taifa hadi lingine.

Msikiti wa Istiqlal jijini Jakarta uliofanyiwa ukarabati mpya, ambao ndio mkubwa zaidi eneo la Kusini Mashariki mwa Asia, uliwakaribisha waumini kwa mara ya kwanza Jumatatu usiku baada ya kufungwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na janga hilo.

Mohamad Fathi, mkazi katika jiji hilo kuu la Indonesia alieleza vyombo vya habari kuwa, Ramadan ya mwaka huu ilikuwa na furaha zaidi kuliko 2020, wakati ambapo watu walipigwa marufuku kushiriki tarawih (sala za jioni).

“Mwaka uliopita kulikuwa na huzuni kwa sababu hatukuruhusiwa kwenda msikitini kwa maombi ya tarawih.”

“Lakini mwaka huu, nina furaha mno hatimaye tunaeza kwenda msikitini kufanya maombi ya tarawih ingawa kuna masharti makali ya kanuni za afya wakati wa sala hizo,” anasema.

Serikali ya taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu walio wengi duniani, imeweka masharti ambapo misikiti inaruhusiwa tu kuwa na asilimia 50 ya waumini.

Waumini pia wanahitajika kuvalia maski na kuzingatia masharti mengine ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo hatari.

Maeneo kadhaa nchini Indonesia yamepiga marufuku mikusanyiko ya watu kushiriki kifungua kinywa huku viongozi wa kidini wakiwahimiza waumini kusalia nyumbani katika baadhi ya sehemu ambapo virusi hivyo vinaongezeka kwa kasi.

You can share this post!

Ramaphosa aitaka Afrika ijitengenezee chanjo ya corona

Mbwa wa Biden kupewa mafunzo mapya