• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
HAKUNA PUMZI

HAKUNA PUMZI

CECIL ODONGO NA CHARLES WASONGA

WAKENYA wanakabiliwa na balaa kuu baada ya serikali jana kukosa kushusha bei ya mafuta, na wakati huo huo ikarefusha kipindi cha kafyu hadi mwisho wa Mei.

Hii ina maana wananchi wanatarajiwa kuendelea kutumia pesa zaidi kugharimia maisha wakati ambao wamepunguziwa fursa za kupata pesa na kupoteza ajira.

Pia imejitokeza kuwa kafyu inayoanza saa mbili jioni katika kaunti za Nairobi, Machakos, Nakuru, Kajiado na Kiambu imegeuka kuwa kichocheo kikubwa cha maambukizi ya corona, kutokana na misongamano ya watu wakielekea nyumbani jioni.

Maelfu ya wakazi wa kaunti hizo wamepoteza mapato kutokana na kulazimika kufunga biashara zao mapema pamoja kuzimwa kwa biashara za hoteli, baa, vituo vya mazoezi na wahudumu wa matatu zinazosafiri nje ya kaunti hizo.

Kulingana na notisi iliyotolewa Jumatatu na Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i, kafyu katika kaunti hizo tano itaendelea kuanza saa mbili kama ilivyo sasa. Katika kaunti zingine itaendelea kuanza saa nne usiku hadi Mei 29.

Haya yamejiri bei ya mafuta ikibakia kuwa ya juu licha ya kilio cha wananchi kuhusu gharama ya maisha kupanda.

Bei ya sasa inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia nane hivi karibuni serikali itakapoanza kutekeleza matakwa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Bei hiyo ya mafuta inaendelea kusababisha kupanda kwa nauli pamoja na bei za bidhaa zingine zinazotengenezwa viwandani, kwani kampuni za usafirishaji na viwanda zinalazimika kuongeza ada zao jinsi bei ya mafuta inavyoongezeka.

Hii inafanyika wakati ambao mamilioni wamepoteza ajira na mapato kutokana na athari za Covid-19, huku serikali ikikosa kuchukua hatua za kuwakinga kutokana na athari hizo.

Hii pia imechangia kuendelea kwa uharibifu wa mazingira raia wengi maeneo ya mashambani na mitaa duni mijini wakilazimika kugeukia matumizi ya makaa na kuni.

IMF YATAKA BEI IPANDE ZAIDI

Ada za stima nazo ziko juu kwa sababu ya kampuni ya Kenya Power kuendelea kutegemea kawi inayotokana na dizeli, licha ya kuwepo kwa kawi ya kutosha inayozalishwa kwa maji na mvuke.

Bei za mafuta hapa Kenya ndizo za juu zaidi Afrika Mashariki, licha ya mataifa kama Rwanda na Uganda kupitishia mafuta yao katika Bandari ya Mombasa.

Hii inafanya wakazi wa maeneo ya mpaka wa Kenya na Uganda pamoja na Tanzania kwenda katika mataifa hayo kununua mafuta.

IMF imekuwa ikitaka Ushuru wa Ziada (VAT) unaotozwa mafuta kuongezwa kutoka kiwango cha sasa cha asilimia nane hadi asilimia 16.

Bei ya juu ya mafuta nchini huwa inasababishwa na kiwango cha juu cha ushuru unaotozwa bidhaa hiyo muhimu.

IMF inataka VAT ya mafuta iongezwe ili kuimarisha kiasi cha fedha ambazo zinakusanywa na Mamlaka ya Ushuru (KRA).

Hitaji la kuongezwa kwa VAT ya mafuta ni moja tu ya matakwa mengi ambayo IMF inataka, hali ambayo itaongeza matatizo kwa mwananchi wa kawaida.

USIMAMIZI DUNI WA UCHUMI

Matakwa mengine ni pamoja na kubinafsishwa kwa mashirika kadhaa ya serikali na kufutwa kazi kwa maelfu ya watumishi wa umma.

IMF imerudi hapa Kenya kutokana na usimamizi duni wa uchumi na mikopo isiyo kikomo chini ya utawala wa Jubilee.

Wakopeshaji hao kutoka ng’ambo walikuwa wamefukuzwa nchini na Rais Mstaafu Mwai Kibaki kwa sera zake za maendeleo ambazo zilitilia mkazo Kenya kutegemea raslimali badala ya kukopa.

Hatua hiyo ilikuwa imeweka Kenya kwenye mkondo wa kujikomboa kutokana na madeni, lakini utawala wa Jubilee umerudisha nchi kwenye minyororo ya IMF na wakopeshaji wengine.

Wakenya walipolalamika mwezi jana kuhusu bei ya juu ya mafuta, serikali kupitia kwa msemaji wake Cyrus Oguna iliwapuzilia mbali ikisema sharti wawe tayari kufadhili shughuli za serikali na maendeleo.

Kampeni ya kupinga mikopo ya kila mara nayo ilikabiliwa kwa msako dhidi ya wanaharakati waliokuwa wakiongoza shinikizo za kuitaka IMF ikome kukopesha Kenya.

Wananchi wanahoji kuwa licha ya viwango vya juu vya ushuru na madeni, kiasi kikubwa cha fedha kinaporwa na maafisa wa serikali wakishirikiana na wafanyibiashara walaghai.

You can share this post!

Mtambue msanii chipukizi anayetunga nyimbo kwa lugha sita...

Njama mpya yachorwa kutimua Ruto Mlima Kenya