• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 1:08 PM
Magavana wahepa suala la ubadhirifu wa pesa za corona

Magavana wahepa suala la ubadhirifu wa pesa za corona

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI za Kaunti zimedai hazijaona ripoti ya Mhasibu Mkuu wa fedha za serikali kuhusu jinsi magavana walivyosimamia utumizi wa mabilioni ya pesa za kupambana na janga la corona.

Ripoti hiyo ambayo inaweza kupatikana katika tovuti ya afisi ya Mhasibu Mkuu, ililaumu karibu kaunti zote kwa usimamizi mbaya wa fedha hizo na ukiukaji wa sheria katika utoaji zabuni za kununua bidhaa na huduma zilizohitajika kupambana na janga hilo mwaka uliopita.

Katika taarifa jana, mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika Baraza la Magavana, Prof Anyang’ Nyong’o, alidai magavana wanasoma tu kuhusu ripoti hiyo katika vyombo vya habari na hivyo basi hawana uwezo wa kujitetea.

“Tunaomba vyombo vya habari kuwa na subira hadi kaunti zitakapopokea ripoti hizo kutoka kwa afisi ya Mhasibu Mkuu, kuzichanganua kisha tutajibu maswali yoyote yatakayoibuka. Serikali za kaunti zinalaumiwa bila kupewa nafasi ya kujitetea wala kuambiwa kama kuna kosa lolote lililofanywa,” akasema.

Ripoti ya Mhasibu Mkuu ambayo ilichapishwa Desemba 2020 na kutolewa kwa umma Februari mwaka huu, ilibainisha kuwa kwa jumla, kaunti zote 47 zilipokea zaidi ya Sh7.7 bilioni kutoka kwa serikali kuu.

Mbali na fedha hizo, serikali za kaunti zilikuwa zimetenga jumla ya Sh5.3 bilioni kutoka kwa bajeti zao, huku Sh849 milioni zikitoka kwa wafadhili.

Mapema wiki hii, maseneta wakiongozwa na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo, walitaka asasi husika zichukulie kwa uzito ripoti hizo na kuadhibu magavana watakaopatikana kufuja pesa za umma.

Miongoni mwa makosa yaliyofichuka katika matumizi ya fedha ni, serikali za kaunti kukosa kufuata sheria katika ununuzi wa vifaa vilivyotakikana, na hivyo kuzua hatari ya ubadhirifu wa fedha.

Kwa mujibu wa Mhasibu Mkuu, hapakuwa na ushahidi wowote kwamba kaunti zilifanya uchunguzi katika soko kabla ya kuamua bei bora ya kununua vifaa kama vile maski na mavazi maalumu ya kusaidia madaktari kujikinga kutokana na maambukizi ya corona.

Kaunti za Embu, Homa Bay, Isiolo na Murang’a zilikosolewa kwa kununua vifaa kutoka kwa wazabuni ambao hawakuhitimu. Kaunti za Busia, Kakamega, Isiolo, Kakamega, Marsabit na Meru zilitajwa kununua vifaa bila kuchunguza bei bora zaidi katika soko. Baadhi ya magavana wamejitetea kuwa, walilazimika kununua vifaa hivyo kwa haraka kwa sababu ya dharura iliyokuwepo.

You can share this post!

‘Uhuru na Raila wanataka kura ya maamuzi upesi’

Wazee waozea jela sababu ya kesi za unajisi