• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Wazee waozea jela sababu ya kesi za unajisi

Wazee waozea jela sababu ya kesi za unajisi

Na TITUS OMINDE

UNAPOINGIA kwenye uwanja wa burudani wa mahabusu katika gereza kuu la Eldoret unakaribishwa na nyuso za wazee wenye umri wa kati ya miaka 60 na 90.

Kulingana na wasimamizi wa gereza hilo kuna wafungwa wakongwe takriban 100 waliohukumiwa kutokana na makosa ya dhuluma za kimapenzi haswa kunajisi watoto.

Idadi kubwa ya wafungwa hao wanahisi kwamba walifungwa kwa makosa ambayo wanadai hawakutenda.

Wakizungumza na Taifa Leo katika gereza hilo walisema kuwa wengi wao walifungwa kwa kukosa pesa za kulipa mawakili walioshughulikia kesi zao.

Wakongwe hao ambao wengi ni wadhaifu kiafya waliomba Bunge kufanyia marekebisho sheria ya dhuluma za kijinsia, iliyoasisiwa na Jaji Njoki Ndung’u.

“Wengi wetu tumehukumiwa kwa makosa ambayo hatukufanya, tuko hapa kutokana na sheria inayotumiwa vibaya kudhalilisha masikini. Tunataka Bunge lirekebishe sheria hii,” akasema Bw Thomas Kimwolo Chelang’a anayetumikia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi.

Kwa sababu ya umri wao na mazingira ya gerezani wanaugua maradhi mbalimbali ya kiumri.

Afisa msimamizi wa gereza la Eldoret, Bw Barnabas Keino, alisema wazee hao wanaugua magonjwa kama vile pumu, upofu miongoni mwa maradhi mengine ambayo huambatana na umri mkongwe.

Aliongeza kwamba wamelazimika kuwapa huduma maalum sababu ya changamoto hizo na zingine zinazohusiana na umri wao.

Mmoja wa wafungwa hao ni Ezekiel Chelimo, 76, ambaye alipofuka wakati anahudumia kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi msichana wa miaka minne katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Chelimo amemwomba Rais kuingilia kati kisa chake ili aachiliwe .

“Natamani kwenda nyumbani; nimezeeka, sina nguvu za kuendelea kutesekea gerezani. Nimekuwa mzigo kwa wafungwa wenzangu na usimamizi wa gereza,” alieleza mzee Chelimo

Hisia zake ziliungwa mkono na Bw Keino ambaye alisema kwa muda ambao mzee huo amekuwa hapo ameonyesha kurekebisha tabia na hivyo kuna haja ya kilio chao kizingatiwe.

“Amekuwa mzigo kwetu. Ni mzee sana kuendelea kuteseka gerezani ikizingatiwa kwamba sasa ni kipofu,” akahoji msimamizi huyo.

Wengi wa wanaume wazee walio jela maisha walihukumiwa kwa makosa ya dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto, mauaji na pia wizi wa mabavu kati ya makosa mengine mazito.

Wanatumikia vifungo vya kati ya miaka saba na 30 huku wengine wakifungwa maisha.

Mfungwa mzee zaidi katika gereza hilo la Eldoret ni Thomas Anduka anayetumikia kifungo cha miaka 10 baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kunajisi.

Wasimamizi wa jela wamewasilisha majina yao kwa Jaji Msimamizi wa Eldoret, Jaji Hellen Omondi, ili kutafakari upya hatima yao.

Jaji Omondi, ambaye alithibitisha kupokea orodha na ombi hilo, alisema kuwa anashauriana na wadau wengine kupata suluhisho mwafaka.

Aliongeza kwamba kuwaachilia wafungwa hao wazee kutategemea ripoti ya kurekebisha tabia zao ambayo haundaliwa na maafisa wa gereza.

Gereza la Eldoret lina takriban wafungwa ikilinganishwa na uwezo wake wa kustahimili wafungwa 700.

“Kuna Idadi kubwa ya wafungwa hapa. Tukijifinya sana tunapaswa kuwa na 800 lakini tumelazimika kuhifadhi karibu 2,000. Hata kuzingatia masharti ya corona ni vigumu sana,” akahitimisha Bw Keino.

You can share this post!

Magavana wahepa suala la ubadhirifu wa pesa za corona

KCB yajiondoa kwenye mashindano ya Bara Afrika ya voliboli...