• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 1:05 PM
Mwanachuo akana kuua familia yake

Mwanachuo akana kuua familia yake

SIMON CIURI na MERCY MWENDE

MWANAFUNZI wa chuo kikuu, Lawrence Warunge, aliyehusishwa na mauaji ya familia yake ya watu wanne na mjakazi mmoja Kiambu, amekanusha mashtaka.

Warunge alisomewa mashtaka kupitia kwa video na Jaji Mary Kasanga jana, ambapo alikana kumuua babake Nicholas Njoroge Warunge, mamake Ann Wanjiku, binamu yake Maxwell Njeka, kakake Christian Njenga Njoroge na mfanyakazi wa shambani James Kinyanjui Wambaa.

Baada ya kukanusha mashtaka, mahakama iliagiza mshtakiwa apelekwe rumande katika gereza la Nairobi hadi Mei 11 wakati kesi itaanza kusikizwa.

Hati ya mashtaka ilieleza kuwa alitekeleza mauaji hayo usiku wa kati ya Januari 5 na Januari 6, mwaka huu katika kijiji cha Karura, Kaunti Ndogo ya Kiambaa.

Alikuwa ametarajiwa kusomewa mashtaka Jumatano lakini upande wa mashtaka ukaomba ruhusa kuthibitisha alikuwa sawa kiakili.

Hii ilikuwa mara yake ya tatu kufanya mtihani huo katika Hospitali ya Mathari, kwani majaribio mawili ya kwanza yalikuwa yameonyesha alikuwa na matatizo ya akili.

Matokeo ya majaribio hayo ya tatu ambayo yaliwasilishwa mahakamani jana, yalithibitisha hana tatizo tena na hivyo basi anaweza kushtakiwa kwa mauaji.

Bi Sarah Muthoni, mpenzi wa Lawrence ambaye awali walikuwa wamepangiwa kushtakiwa pamoja, aliachiliwa huru Januari 26 na sasa atakuwa shahidi anayetegemewa na upande wa mashtaka.

Kwingineko, Kiongozi wa Mashtaka katika mahakama iliyo mjini Nyeri amemruhusu afisa wa zamani wa jeshi Peter Mwaura Mugure ajiwakilishe katika usikilizaji wa kesi ya mauaji.

Alipokuwa akijibu ombi lililowasilishwa mahakamani na Bw Mugure, Kiongozi wa Mashtaka Duncan Ondimu alisema halipingi ombi la mshtakiwa la kujiwakilisha katika kesi hiyo anayokabiliwa na mashtaka matatu ya mauaji.

Hata hivyo, Bw Ondimu alimwonya mtuhumiwa kuhusu hatari ya kujiwakilisha katika kesi anayoweza kuadhibiwa kwa kifungo cha maisha gerezani.

Wakati huo huo, mbele ya Hakimu Florence Muchemi, Bw Ondimu alikataa kumrudishia mshtakiwa gari lake kama alivyoomba.

Alieleza, gari la mwanajeshi huyo litatumika kama ushahidi katika kesi.

“Mshtakiwa alilitumia gari hilo kusafirisha miili ya mkewe marehemu Joyce Syombua na watoto wake wawili Shanice Maua na Peter Mwaura kutoka kwa Kambi ya Jeshi la Laikipia hadi kwenye makaburi alipowazika,” akasema Bw Ondimu.

Aliiomba pia mahakama iikatae ombi la mwanajeshi lililotaka awachiliwe kwa dhamana.

Kulingana na Bw Ondimu, mshtakiwa hakutoa ushahidi wowote mpya utakaobadilisha hukumu ya awali wa mahakama iliyomnyima dhamana.

Katika hati ya kiapo iliyoandikwa na afisa mpelelezi Reuben Mwaniki, alieleza mahakama ilimnyima mshukiwa dhamana kwa sababu alijaribu kuingilia uchunguzi wa kesi hiyo.

Bw Mugure alikuwa ameomba mahakama imruhusu ajiwakilishe baada ya kuwafuta kazi mawakili wake watatu.

Mshtakiwa anatuhumiwa kwa kumuua mkewe Syombua mwenye umri wa miaka 31 na watoto wao wawili wenye umri wa miaka 10 na mwingine tano.

Alishtakiwa pamoja na mfanyikazi wake wa Kibarua Bw Collins Pamba mnamo Oktoba 26, 2019 katika Kambi ya Jeshi ya Laikipia mjini Nanyuki. Bw Pamba amezuiliwa katika Gereza Kuu la Kerugoya.

Kesi itaendelea mnamo Mei 20.

You can share this post!

Matokeo ya somo la Kiswahili yaimarika pakubwa

NASAHA: Tujipinde zaidi kwa uchaji Mungu katika Mwezi huu...