• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Msako wa baharini wapunguza samaki

Msako wa baharini wapunguza samaki

Na KALUME KAZUNGU

UHABA wa samaki unashuhudiwa kwenye miji mbalimbali ya Kaunti ya Lamu tangu mwezi mtukufu wa Ramadhani ulipoanza rasmi Jumatano.

Uhaba huo wa samaki unashuhudiwa kwenye visiwa vya Lamu na Shella na pia miji ya Mokowe, Hindi, Faza, Pate na Kiunga.

Inatarajiwa hali sawa na hii itatokea katika kaunti nyingine zinazotegemea samaki wanaovuliwa Lamu.

Hali hiyo inaaminika kuchangiwa na operesheni iliyozinduliwa majuma mawili yaliyopita inayolenga kuwanasa wavuvi wanaotumia vifaa vilivyoharamishwa kuvua samaki kwenye bahari Hindi kote Lamu.

Kufikia sasa tayari wavuvi zaidi ya 20 wamekamatwa na kufikishwa kortini ilhali nyavu na mashua zao zikizuiliwa na walinda usalama.

Wakizungumza kisiwani Lamu Alhamisi, wachuuzi wa samaki walikiri kukosa shehena za bidhaa hiyo kwani wavuvi waliowategemea wamesusia shughuli baharini kwa kuhofia kulengwa na walinda usalama.

Mchuuzi tajika wa samaki katika kisiwa cha Lamu, Mustafa Shafi, alisema majokofu yake yamesalia bila chochote kwani samaki wameadimika tangu juma hili lilipoanza.

Bw Shafi aliiomba serikali kusitisha msako wa wavuvi baharini kwani ulizinduliwa wakati usiofaa.

“Huu ni wakati wa kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo mlo wa samaki ni muhimu kwa kufungulia saumu jioni. Isitoshe, janga la Korona limeathiri shughuli nyingi, ikiwemo uvuvi. Itakuwaje leo serikali ianzishe operesheni ya kuhangaisha wavuvi wetu? Samaki hakuna kwani wavuvi wamekamatwa ilhali wengine wakiogopa kuingia baharini. Wasikie kilio chetu. Tunaumia,” akasema Bw Shafi.

Mvuvi Omar Athman alisema alilazimika kusitisha uvuvi baharini baada ya kuchoshwa na mahangaiko ya polisi.

Alisema familia yake ambayo hutegemea uvuvi kwa sasa inateseka.

Bw Athman aliiomba serikali kusambazia wavuvi wa Lamu chakula cha msaada ili kukimu familia zao baada ya kitega uchumi chao kukatizwa.

“Utalii na biashara vimefifia kutokana na janga la Covid-19. Kilimo hakuna hapa Lamu. Tumetegemea uvuvi pekee kukimu mahitaji ya familia. Kwa nini serikali inatuhangaisha wakati huu wa janga la Korona? Ningesihi operesheni inayoendelea isitishwe ili tuendelee na shughuli zetu kama kawaida,” akasema Bw Athman.

Bi Mwanasomo Hamisi, anasema amelazimika kufunga kibanda chake hasa baada ya wavuvi ambao tayari alikuwa amewalipa kumletea samaki kutiwa mbaroni na walinda usalama.

“Nilikuwa nimelipia shehena yangu ya samaki kwa wavuvi mapema. Nilichosubiria ilikuwa ni mzigo wa kuendeleza biashara yangu. Nasikitika kwamba fedha zangu zimepotea hivyo baada ya niliowalipa kukamatwa baharini,” akasema Bi Hamisi.

Bi Hawa Salim alisema amelazimika kusaka samaki wa kununua, ambapo wale wachache aliobahatika kupata aliwanunua kwa bei ghali.

“Kawaida kilo ya samaki ni Sh 300. Nimenunua samaki leo kwa Sh 500 kwa kilo. Samaki wenyewe hawatoshi. Nimeongeza na ng’onda ili mlo wetu wa jioni tukifungua Ramadhani uwe wa kutosha,” akasema Bi Salim.

Mkurugenzi wa Idara ya Samaki, Kaunti ya Lamu, Ali Ahmed aidha alisema majadiliano yanaendelea kwenye ofisi yake ili kuona ni hatua gani mwafaka zitakazowezesha wavuvi wa Lamu kuendeleza shughuli zao bila kutatizwa.

Naye Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, alisema ofisi yake imeandaa kikao na wavuvi wote wa Lamu Ijumaa wiki hii ili kujadiliana ni jinsi gani uvuvi utaendelezwa, japo kwa kufuata masharti yanayoambatana na sheria za uvuvi baharini.

“Tutakaa tujadiliane ili wavuvi watupe kauli yao na sisi pia tutoe msimamo wetu ili uvuvi uendelee kwa kufuata sheria zote zinazohitajika,” akasema BwMacharia.

You can share this post!

NASAHA: Tujipinde zaidi kwa uchaji Mungu katika Mwezi huu...

Jaji ataka mkewe alipwe mshahara akiwa Jaji Mkuu