• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 PM
Nikipata fursa kuwa Rais sitamhangaisha naibu wangu – Ruto

Nikipata fursa kuwa Rais sitamhangaisha naibu wangu – Ruto

Na SAMMY WAWERU

NAIBU wa Rais Dkt William Ruto amekiri uhusiano wake na Rais Uhuru Kenyatta una doa kwenye mahojiano na runinga moja humu nchini.

Dkt Ruto amesema hilo kufuatia kuendelea kutengwa katika maamuzi ya mipango na mikakati muhimu serikalini.

Alisema baada ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa Machi 2018 kupitia salamu za maridhianomarufu kama Handisheki, majukumu aliyokuwa akitekeleza yalielekezwa kwa viongozi wengine.

Akieleza kuheshimu uamuzi wa Rais, alisema alipokonywa wajibu wake kama Naibu wa Rais kumshauri.

“Kati ya 2013 na 2017 tulishirikiano kuongoza nchi, kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo, ila baada ya Handisheki Rais aliona ni vyema apate ushauri kutoka kwa wengine. Huo ni msimamo na uamuzi wake na ambao nina uheshimu,” Dkt Ruto akasema.

Uhusiano wa viongozi hao wawili na ambao kipindi cha kwanza cha uongozi walionekana kushirikiana sako kwa bako, ikiwemo kuvalia mavazi yanayowiana wanapojitokeza kwa umma, unaendelea kudorora.

Rais Kenyatta na wandani wake wamekuwa wakimlaumu Dkt Ruto kwa kuanza kampeni za mapema kuingia Ikulu 2022.

Naibu Rais hata hivyo alisema hajabadilisha mkondo wake wa uongozi, akieleza ni mtazamo wa Rais na ambao anauheshimu kwa sababu ni wa hiari.

“Ikiwa kuna kiongozi ambaye ameheshimu bosi wake faraghani na machoni mwa umma ni mimi. Nitaendelea kumheshimu na kutekeleza majukumu anayonipa,” akasema.

Aidha, Dkt Ruto alisema endapo 2022 atapata fursa ya kuongoza Kenya atamheshimu naibu wake.

“Kufuatia masaibu ninayopitia, ninaelewa jinsi manaibu wa rais huhangaishwa. Nikipata nafasi kuongoza nchi nitamheshimu naibu wangu,” akasema.

Tangu janga la Covid-19 litue nchini, Dkt Ruto alidai hajakuwa akihusishwa katika mipango na mikakati kuliangazia.

You can share this post!

Jaji ataka mkewe alipwe mshahara akiwa Jaji Mkuu

Timu tatu za voliboli kukosa mastaa kwenye kipute muhimu