RAILA AMTATIZA UHURU AKILI

Na MWANDISHI WETU

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga, ameonekana kuandama mipango inayomlazimu Rais Uhuru Kenyatta kujikuna kichwa katika jitihada za kujaribu kung’amua karata yake kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022.

Duru zinasema kwamba Bw Odinga amekuwa akichukua hatua zinazomuacha Rais Kenyatta na washirika wake wa kisiasa wamechanganyikiwa kuhusu mwelekeo atakaochukua kabla na katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Viongozi hao wawili wamekuwa na uhusiano mwema tangu handisheki yao ya Machi 9, 2018 iliyotuliza nchi na kumwezesha Rais Kenyatta kutawala bila upinzani hadi juzi miungano ya kisiasa ilipoanza kujitokeza.

Handisheki hiyo ilizaa mchakato wa kubadilisha katiba wa BBI. Uhusiano wao wa kisiasa ulimfanya Rais Kenyatta kumtenga Naibu Rais William Ruto serikalini na katika chama cha Jubilee.

Bw Odinga ameonekana kumchangamkia Dkt Ruto ambaye mbali na kutengwa serikalini, walitofautiana vikali kuhusu handisheki na BBI.

Siku chache tu baada ya kuibuka ripoti kwamba Bw Odinga na Dkt Ruto walikuwa wakizungumza kwa lengo la kuungana, waziri huyo mkuu wa zamani alionekana na Rais wakikagua miradi jijini Nairobi.

Wadadisi walisema hii ilikuwa mbinu ya kumtuliza Bw Odinga. ODM ilisema kwenye taarifa kwamba handisheki ilikuwa ingali imara na kwamba dhamira yake ni kufanikiwa kwa mswada wa kubadilisha katiba wa BBI utakaowezesha kufanyika kwa kura ya maamuzi.

Hali ilipoonekana kurejea kawaida, naibu kinara wa ODM Wycliffe Oparanya alikutana faraghani na Dkt Ruto kujadili ushirikiano wa naibu rais na Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Siku mmoja baada ya kukutana na Dkt Ruto, Bw Oparanya alikutana na Bw Odinga nyumbani kwake Karen, Nairobi na akakiri kwamba alimjuza aliyozungumza na Naibu Rais.

Matukio hayo yalimfanya Rais Kenyatta na washirika wake kujikuna kichwa kujaribu kuelewa anayopanga Bw Odinga.

Baadhi ya wadadisi wanasema kwamba ni hali hii iliyomfanya Rais Kenyatta kumtuma kaka yake mdogo Muhoho Kenyatta na mwenyekiti wa Kanu, Bw Gideon Moi kwa Bw Odinga kumshawishi asijiunge na Dkt Ruto. Bw Moi ni mmoja wa vinara wa muungano wa One Kenya Alliance pamoja na Kalonzo Musyoka wa Wiper, Musalia Mudavadi wa ANC na Moses Wetangula wa Ford Kenya.

“Kuna uwezekano kwamba baada ya mkutano kati ya Oparanya na Dkt Ruto, Rais anahisi muungano kati ya naibu wake na Bw Odinga unasukwa, ishara kwamba balozi huyo wa miundomsingi Afrika (AU)haridhishwi na hali ya handisheki na zaidi ya yote One Kenya Alliance. Hii ndiyo sababu alimtuma Muhoho na Moi kwa Bw Odinga wamshawishi atafakari kuhusu hatua yake,” asema mdadisi wa siasa Susan Chebet.

Haikubainika mara moja iwapo ni Rais aliyewatuma wawili hao kwa Bw Odinga.

Wadadisi wanasema kwamba kufuatia ishara ambazo Bw Odinga amekuwa akitoa, Rais Kenyatta lazima anajitahidi kumhakikishia kuwa anaheshimu handisheki na kuondoa mkono wake katika One Kenya Alliance.

Ingawa Bw Odinga hajatangaza hadharani iwapo atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, wandani wake wamekuwa wakiashiria kwamba alinuia kutegemea uhusiano wake na Rais Kenyatta kuingia ikulu hapo mwakani.

Kulingana na ODM, Bw Odinga hakuwasilisha ombi la kuwania tiketi ya chama hicho ya kugombea urais. Bodi ya uchaguzi ya chama hicho ilisema muda wa kuwasilisha maombi ulipokamilika Machi 30 mwaka huu, ni magavana Ali Joho ( Mombasa) na Wycliffe Oparanya pekee ambao walikuwa wamefanya hivyo.

Wadadisi wanasema hii imewafanya wanaopanga mikakati ya siasa za urithi mwaka wa 2022 kujikuna kichwa.

Rais Kenyatta na Bw Odinga walisema kwamba handisheki yao haikuhusu uchaguzi mkuu wa 2022, lakini wadadisi wanasema kuna kila dalilli kwamba waziri huyo mkuu wa zamani amewachanganya wanaopanga siasa za urithi.

Wanasema kwamba kabla ya chaguzi ndogo za Machakos, Matungu na Kabuchai, uhusiano wa vinara hao wa handisheki ulikuwa shwari huku Bw Odinga akipigia debe Mswada wa kura ya maamuzi wa BBI.

“Mambo yaliharibika baada ya mswada huo kupitishwa na mabunge ya kaunti na kisha muungano wa One Kenya Alliance kuzaliwa kutoka kwa chaguzi ndogo za Matungu, Kabuchai na Machakos ambao ulimtenga Bw Odinga na kusemekana kuwa na baraka za Rais Kenyatta,” asema mbunge wa chama cha ODM ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Susan Mugwe, mkutano wa Bw Odinga, Muhoho na Moi ulinuia kufanya watu kuamini kwamba handisheki ingali imara.

Habari zinazohusiana na hii

Wapuuza Uhuru