• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
JAMVI: Magavana ‘wanaofunga kazi’ wang’ang’aniwa na Uhuru na Ruto, kulikoni?

JAMVI: Magavana ‘wanaofunga kazi’ wang’ang’aniwa na Uhuru na Ruto, kulikoni?

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta na Naibu wa Rais William Ruto sasa wanang’ang’ania uungwaji mkono wa magavana watakaostaafu mwaka ujao.

Tangu Rais Kenyatta kupiga marufuku mikutano ya kisiasa mwezi uliopita kufuatia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini, Naibu wa Rais Ruto ameimarisha juhudi za kutaka kuwavutia magavana wanaohudumu kipindi cha mwisho upande wake.

Alhamisi iliyopita, Bw Obado alikutana na Gavana wa Nandi Stephen Sang – ambaye ni mwandani wa Naibu wa Rais – nyumbani kwake katika eneo la Rapogi, Kaunti ya Migori. Gavana Obado tayari ametangaza kugura ODM na sasa ameanza kuimarisha umaarufu wa chama chake cha People Democratic Party (PDP).

Wandani wa kiongozi wa ODM Raila Odinga, mwezi uliopita, walidai kuwa kuna uwezekano Bw Obado anatumiwa na muungano wa One Kenya Alliance (OKA) unaoungwa mkono na Rais Kenyatta, kuhujumu waziri mkuu wa zamani.

Lakini ziara ya Gavana Sang nyumbani kwa Bw Obado ni ishara kwamba huenda kiongozi huyo wa Migori anaelekea kwa Naibu wa Rais Ruto.

Naibu wa Rais tayari amekutana na magavana zaidi ya 20 ndani ya wiki tatu zilizopita katika juhudi za kutafuta uungwaji mkono 2022.

Baadhi ya magavana wanaohudumu muhula wa pili na wa mwisho, wanalenga kuwania useneta na ubunge huku wengine wakimezea mate uwaziri na nyadhifa nyinginezo za juu katika serikali ijayo.

Gavana wa Turkana Josphat Nanok anayemalizia muhula wake wa pili na aliyekuwa waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri wamekuwa wakikutana na magavana mbalimbali kwa niaba ya Dkt Ruto.

Naibu wa Rais pia amekutana na magavana kadhaa, akiwemo Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye ni mwandani wa Bw Odinga.

Baadhi ya magavana wameepuka kujihusisha na Dkt Ruto kutokana na hofu ya kufunguliwa mashtaka au kuhangaishwa na serikali. Magavana wanaohudumu muhula wa mwisho wanahisi kuwa itakuwa rahisi kupata wadhifa serikali iwapo Dkt Ruto atashinda urais 2022.

Mezea mate

Lakini kundi jingine la magavana linahisi kuwa muungano wa OKA endapo utaungwa mkono na Rais Kenyatta huenda ukafanikiwa kuunda serikali ijayo. Miongoni mwa magavana wanaomezea mate nyadhifa katika serikali ijayo ni kiongozi wa Busia Sospeter Ojaamong ambaye anasema kuwa yuko tayari kuhudumia taifa katika wadhifa wowote baada ya kukamilisha mihula yake miwili.

“Mpango wa Maridhiano (BBI) unapendekeza kuongezwa kwa nyadhifa serikalini. Iwapo BBI itapitishwa, basi niko tayari kuhudumia nchi hii katika wadhifa wowote,” Bw Ojaamong aliambia Taifa Jumapili.

Kiongozi huyo wa Busia pia alidokeza kuwa huenda akawania useneta katika Uchaguzi Mkuu ujao. Rais Kenyatta amekuwa akikutana na magavana wa maeneo yanayodhaniwa kuwa ngome za Bw Odinga kama vile Magharibi, Nyanza na Pwani.

Mwezi uliopita, Rais Kenyatta alikutana na magavana Hassan Joho (Mombasa) Amason Kingi (Kilifi) ana Salim Mvurya wa Kwale ambapo waliafikiana kuunda chama kitakachotetea masilahi ya wakazi wa Pwani.

Chama kipya cha Pwani kinatarajiwa kuzinduliwa baada ya mfungo wa Ramadhan, mwezi ujao.

Mkutano huo wa Rais Kenyatta na viongozi wa Pwani umezua tumbojoto ndani ya kambi ya Bw Odinga.

Viongozi wa ODM waliozungumza na Taifa Jumapili na kuomba wasitajwe kutokana na hofu ya kusutwa, walidokeza kwamba kuna njama ya kutaka kumtenga Bw Odinga.

“Ni kweli, kuna baadhi ya watu ambao wameunda njama ya kutaka kumaliza umaarufu wa kiongozi wa chama katika baadhi ya maeneo ambayo ni ngome za ODM. Hatutakubali na tuko chonjo,” akasema mmoja wa viongozi wa ODM.

Alisema Bw Odinga anapanga kuanzisha kampeni kali ya kujipigia debe katika maeneo mbalimbali ya nchi baada ya kupona.

Naibu wa Rais anashikilia kuwa muungano wa OKA hauna uwezo wa kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu ujao bila kuungwa mkono na Bw Odinga.

Muungano wa OKA unajumuisha kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, Gideon Moi (Kanu), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya).

Seneta wa Elgeyo Marakwet Murkomen Kipchumba pia amedokeza kuwa Dkt Ruto ameanzisha juhudi za kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa Bw Odinga.

“Dkt Ruto akiungana na Bw Odinga hakutakuwa na uchaguzi kwani atakuwa ameshinda hata kabla ya kupiga kura,” akasema Bw Murkomen.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kuwa wanasiasa wangali wanajipanga hivyo ni vigumu kutabiri mirengo yao kwa sasa.

“Wanasiasa wangali wanajipanga; tutaona miungano thabiti kuanzia Januari mwaka ujao. Kwa sasa hawatabiriki; leo wanakutana na Naibu wa Rais na kesho wanakutana na Rais Kenyatta,” anasema Prof Medo Misama, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

You can share this post!

JAMVI: Njama ya Raila kubomoa One Kenya Alliance

JAMVI: Mkanganyiko mkuu unaogubika siasa za urithi Pwani