• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
KINYUA BIN KING’ORI: Rais Suluhu ametoa ishara atafanikisha demokrasia TZ

KINYUA BIN KING’ORI: Rais Suluhu ametoa ishara atafanikisha demokrasia TZ

Na KINYUA BIN KING’ORI

Tangu kifo cha aliyekuwa Rais wa taifa jirani la Tanzania Marehemu John pombe magufuli aliyetisha kila mtu nchini humo wakiwemo viongozi wa upinzani, na ulimwenguni kwa jumla kando na wananchi wa Tanzania.

Kwa Sasa, wanatazama na kufuatilia kwa ukaribu mno mbinu mpya atakazotumia Rais mpya Bi Samia suluhu Hassan.

Wananchi wengi wa jamhuri ya Tanzania wana wingi wa matumaini Rais Suluhu ataibuka na dawa mujarabu kuimarisha uchumi wa taifa, kupanga mikakati kabambe ya kukabili maradhi ya Corona, kupambana na wafisadi sawia kustawisha demokrasia. Hivyo, kila hatua anayochukua huenda ikaumiza au kuwaletea matunda ya ufanisi raia wa Watanzania.

Rais huyo aliyeingia katika historia kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa nchi hiyo, anafaa kutambua kibarua kilicho mbele yake wala asitarajie mambo yawe papai juu ya kijiko. Atahijitajika kujikaza kisabuni kuthibitishia umma haikuwa bahati nasibu kwake kuwa Rais bali aliyestahiki wadhifa huo wenye hadhi ya juu.

Sina shaka, kiongozi huyo atatumia uzoevu wake serikalini kuendeleza rekodi ya marehemu magufuli ya kutetea na kulinda maslahi ya wananchi wanyonge japo kwa kuzingatia haki na katiba.

Tayari ameanza kutekeleza majukumu yake vyema na kutoa magizo mengi na kweli ikiwa huo ndio mtindo wake wa uongozi ambao ataendelea kuzingatia huenda akawa Rais wa kwanza kupalilia mfumo wa demokrasia nchini humo na kuleta uhuru, uwazi, haki na katiba inayojali Watanzania wote.

Viongozi wa upinzani kwa kipindi cha Magufuli wameishi wakihangaishwa, kutishwa, kuteswa, kudhulumiiwa kiasi cha wengine kuwa wakimbizi wa kisiasa katika mataifa ya kigeni.

Vyombo vya habari vilivyokwenda kinyume na kuonekana kukosoa utendekazi kazi wa serikali walijikuta matatani hata kufungiwa.

Inatia moyo kwamba Rais Suluhu ameleta suluhu kwa kuagiza vyombo vya habari ambavyo vilifungwa na mtangulizi wake vifunguliwe na wahusika waruhusiwe kuendeleza shughuli zake kwa kuzingatia Sheria za nchi.

Licha ya mama huyo kukaa mamlakani kwa muda mfupi, anapaswa kupongezwa kwa kukubali kuongoza si kupitia ubabe wa kujipiga kidari na udikteta, bali kwa kukumbatia sheria na kuheshiimu haki za raia wote bila ubaguzi.

Ingawa Rais magufuli alipuuza janga la Corona, Rais Suluhu ameonyesha kukubali kuna hatari kwa raia wa Tanzania kuendelea kuangamizwa na homa hiyo hatari ikiwa serikali itaendelea kufanyia maradhi hayo dhihaka.

Rais Suluhu amefanyia Watanzania hisani kubwa kujitolea kukiri ugonjwa wa Corona upo na kuunda kamati ya wataalamu yenye azma ya kutathmini kwa kina janga la covid-19 ambapo watashauri serikali na wananchi mikakati muhimu na kanuni zinazofaa kubuniwa kuzuia msambao na jinsi gani serikali itawafaa wananchi wanaoambukizwa ugonjwa huo.

Tamati, naomba Rais huyo wa Tanzania ajue Watanzania na walimwengu mzima wanatarajia chini ya uongozi wake upinzani utapewa usikivu, katiba itaboreshwa, uchumi utapanuka, miundo msingi itaimarishwa na demokrasia kupewa nafasi shtahiki na atakomesha hulka ya viongozi kuonekana kama watekaji nyara kwa kudhibiti mamlaka ya asasi kama Bunge na mahakama ili kukandamiza haki za raia wengine kwa kujilimbikizia mamlaka.

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: Mitandao yabadili sura ya maandamano nchini

Wamaragoli wanaoishi Uganda watarajiwa kutambuliwa rasmi