• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
‘Tutakupeza Prof Ken Walibora’

‘Tutakupeza Prof Ken Walibora’

Na Hosea Namachanja

Mauti yangalikuwa binadamu, ningalijihimu na niyaulize ni kitita kipi cha hela yangalitaka lakini tatizo, mauti si binadamu.

Aidha, yangalikuwa yaongea na kula kama mimi, mlo mzuri ningeyaandalia na kuyarai yatuachie mtoto wa mwalimu uhai wake lakini yote tisa, twakubali yaishe.

Katika udogo wake, alitamani kuwa askari na avalie magwanda mazuri kama askari. Alitamani akiwa, akue mdogo zaidi, ili atoshee redioni kama alivyodhania wanahabari walikuwa na zaidi ya hayo, alitamani sauti yake isikike redioni na asikilizwe na wasikilizaji kama alivyokuwa akisikiliza.

Profesa Walibora, alikuwa na ubongo wa hekima, kifuani alijawa na moyo wa ushujaa na kinywani ulimi wa ufasaha. Kama desturi yake, aliyasema maneno na kuwaacha watu wengine watende matendo lakini alitenda matendo na kuacha watu wengine waseme maneno.

Akiwa mwanahabari NMG ambapo ilikuwa mojawapo ya ndoto ya utotoni, alikizoeza kipaji chake cha uanahabari hadi kila alipotaka kukitumia, kilikuwa tayari kutumika.

Katika lugha ya Kiswahili, alikuwa kama Sheikh Shaaban Roberts nchini mwetu. Kwenye makala Kina cha Fikra na Kauli ya Walibora, alikishabikia Kiswahili kwa jino na ukucha.

Baadhi ya michango yake ; ubunifu wa istlahi “eneobunge” na falsafa, “tusipiganie fito, tunajenga nyumba moja” katu haitofutika. Riwaya pendwa, Siku Njema, itazidi kuwa kumbukumbu maishani mwetu kama riwaya ya kwanza ya mkenya ya Kiswahili kuwahi kutahiniwa nchini.

Vipaji, alivilea. Si kwa uandishi si kwa uanahabari. Hakika, mti mkuu ukigwa, wana wa ndege huyumba. Nikiwa katika maandalizi ya kumtaka anifafanulie zaidi kuhusu istilahi “kidijiti” kwa maana ya “digital” wakati binafsi nilijua kama “dijitali”, mauti yalimchukua mtoto wa mwalimu. Huzuni.

Liniumalo zaidi, nilikuwa tu nimepata namba yake ya simu ili anilee nami nije niwe kama yeye na kifo kikamchukua nikasalia na namba ambayo kila nilipoiangalia, machozi yalinibubujika usoni. Nilikosea wapi?

Ulalapo pema Prof Walibora, kumbuka hati na wino wako hadi sasa, hamna kilichofutika. Sote tulio hai, tutazidi kukilea Kiswahili kuanzia pale mkono wako ulipokwamia na kuyasoma maandishi yako milele. Twamuomba Mungu, azidi kuilaza roho yako pahali pema patakatifu. Amina.

 

You can share this post!

ARVs: Makanisa yaunga usambazwaji wa haraka

Mamia wauawa mpakani mwa Ethiopia na Somalia