• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
TAHARIRI: Unyama wa polisi si dawa ya corona

TAHARIRI: Unyama wa polisi si dawa ya corona

KITENGO CHA UHARIRI

UTEKELEZAJI wa kanuni za kudhibiti maambukizi ya corona umekuwa na pandashuka zake.

Katika kaunti tano zilizowekewa muda wa mapema wa kafyu, kila jioni hushuhudiwa foleni ndefu za magari barabarani, yakielekea mitaa mbalimbali. Jijini Nairobi hali huwa mbaya zaidi. Wenye magari wanaotoka ofisini saa kumi na moja za jioni hufika mitaani baada ya saa tatu za usiku.

Barabara zote huwa na mistari hiyo, hasa ile ya Mombasa, ambayo imefungwa katika sehemu kadhaa.

Lakini pia kuna Wakenya ambao kwa kupenda tu, au kimakusudi, huamua kuingia barabarani zikiwa zimekabia dakika chache kufika wakati wa kafyu.

Huenda ni kutokana na dhana hii ambapo usiku wa Jumamosi, maafisa wa polisi waliodai kupokea maagizo kutoka kwa wakubwa wao, waliwahangaisha wananchi karibu usiku kucha kwenye vizuizi vya barabarani.

Kwa kuwazuilia watu kwenye vizuizi hivyo, huenda polisi walikusudia kuwapa funzo maelfu ya Wakenya ambao hujipata nje baada ya saa mbili za jioni, katika kaunti za Nairobi, Kiambu, Machakos, Nakuru na Kajiado.

Lakini polisi walionyesha kukosa busara walikataza hata magari ya kubeba wagonjwa. Ambalensi zilizokuwa zikisafirisha wagonjwa pia zilikatazwa kupita, na hivyo kuhatarisha maisha ya wengi, jambo ambalo serikali ilijitia hamnazo.

Watu waliokuwa wakipeleka watoto wachanga hospitalini, wagonjwa waliokuwa na miadi na madaktari na hata watoaji huduma muhimu walikatazwa kuendelea na safari.

Madaktari, wauguzi, wanahabari na wasafirishaji wa vyakula hawakusazwa kwenye tukio hilo.

Msemaji wa Serikali Kanali Mstaafu Cyrus Oguna, alitetea kitendo hicho akidai kilifaa kuwa funzo kwa Wakenya wanaopenda kupuuza kanuni za kuzuia maambukizi ya corona.

Hata kama ni kweli kuna Wakenya wasiotii kanuni, basi mbona kuzuia ambalensi na madaktari, ambao jukumu lao ni kusaidia kuokoa maisha? Kwenye msongamano huo wa watu, walikaribiana na kufanya kanuni za kukaa umbali wa mita moja zisitimizwe.

Polisi wakabiliane na watu wanaovunja kanuni za kafyu, lakini walio na vibali na wenye dharura za kiafya wasihangaishwe. Ugonjwa wa corona hautamalizwa kwa kufuata maagizo kutoka juu.

You can share this post!

Nketiah aokotea Arsenal pointi moja dhidi ya Fulham katika...

WARUI: Matokeo ya mtihani wa KCPE yanazua maswali kadhaa