• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
UDAKU: Foden kijogoo! Anawika uwanjani na chumbani pia

UDAKU: Foden kijogoo! Anawika uwanjani na chumbani pia

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO mvamizi wa Manchester City, Phil Foden, anatarajia kuitwa baba kwa mara nyingine baada ya kuthibitisha kuwa amecheka tena na nyavu za mchumba wake, Rebecca Cooke.

Mwanasoka huyo raia wa Uingereza alikuwa mzazi akiwa na umri wa miaka 18. Hii ni baada ya uhusiano wake na Rebecca, ambaye pia ana umri wa miaka 20 kwa sasa, kujaliwa mtoto wa kiume, Ronnie, mnamo Januari 2019. Ronnie ni jina la utani ambalo Foden alipagazwa na wenzake katika akademia ya Man-City.

Kupitia mtandao wa Instagram wiki jana, Foden aliwafichulia mashabiki wake kwamba Rebecca ameanza tena kuhudhuria kliniki na wanatarajia kimalaika cha kike mwezi Agosti.

“Familia itapanuka hivi karibuni. Tunatarajia mgeni wa kike atakayetufungulia rasmi msimu mpya wa 2021-22,” akaandika Foden chini ya picha aliyopigwa pamoja na Rebeccal wakiwa mbele ya kasri lao la Sh455 milioni mjini Prestbury, Uingereza.

“Foden ni jogoo! Anazidi kuwika uwanjani na chumbani. Hachoki kufunga mabao – ndani au nje ya uwanja. Amekuwa nguzo kubwa kambini mwa Man-City na huenda akamaliza kampeni za msimu huu wa 2020-21 akiwa na mataji matano – manne ya uwanjani na moja kutokana na mchezo wa siri chumbani!” akatania fowadi chipukizi wa Manchester United, Mason Greenwood, kwenye Instagram.

Foden na Greenwood, 18, waliwahi kutimuliwa pamoja katika timu ya taifa ya Uingereza kwa kukiuka masharti ya kudhibiti msambao wa virusi vya corona, kikosi hicho kilipokuwa kikijiandaa kuvaana na Iceland ugenini kwenye gozi la UEFA Nations League mnamo Septemba iliyopita.

Uingereza waliibuka washindi wa mechi hiyo kwa 1-0 mjini Reykyavik.

Vyombo vya habari Iceland vilidai kwamba Foden na Greenwood walihepa katika hoteli ambayo wanasoka wa Uingereza walikuwa wametengewa, na kwenda kuburudika na makahaba wawili wakongwe katika hoteli nyingine tofauti usiku kucha.

Kila mmoja wao alitozwa faini ya Sh194,000 kwa kosa hilo lililotishia kusambaratisha uhusiano wa Foden na Rebecca.

Foden alifunga bao katika ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Man-City dhidi ya Borussia Dortmund kwenye mkondo wa pili wa robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), mnamo Jumatano iliyopita nchini Ujerumani.

Ufanisi huo uliwapa Man-City tiketi ya kuchuana na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwenye hatua ya nusu-fainali, baada ya kudengua Dortmund kwa jumla ya mabao 4-2.

Mbali na kupigiwa upatu wa kutia kapuni ufalme wa UEFA, Man-City wako pazuri zaidi kunyanyua taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), League Cup na Kombe la FA chini ya kocha Pep Guardiola muhula huu.

You can share this post!

DIMBA: Huyu Vitinha wa Wolves kama ferari, akitoka unyoya...

UDAKU: Melanie awachoka visura kudonadona penzi lake na...