• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 3:17 PM
Moi sasa aweka mikakati imara kutua Ikulu 2022

Moi sasa aweka mikakati imara kutua Ikulu 2022

STANLEY KIMUGE na ONYANGO K’ONYANGO

KIONGOZI wa chama cha Kanu, Gideon Moi, anaendelea kuweka mikakati maridhawa ili kuhakikisha kwamba anaingia ikulu Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu mwaka 2022.

Bw Moi, ambaye ni mwanawe rais wa pili marehemu Daniel Moi, sasa analenga kusaka umaarufu maeneo mbalimbali nchini kando na himaya yake ya kisiasa ya Bonde la Ufa, anakokabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Naibu Rais Dkt William Ruto.

Mnamo Ijumaa wiki jana, Bw Moi alikutana na wabunge Hassan Oda (Isiolo Kaskazini), Ali Guyo (Garsen), Sofia Adan (Marsabit) Hiribae Buya (Galole) na Wario Gufu (Moyale).

Mkutano huo unadaiwa kuhakikisha kuwa anasaka uungwaji mkono kutoka eneo la Kaskazini Mashariki na jamii ya wafugaji, ambao kwao chama cha Kanu bado ni maarufu sana.

“Tunaendelea kushirikiana na viongozi wengine ili kuunda umoja na muungano ambao utawezesha watu wetu wafahamu mengi kuhusu haki zao na kiongozi bora atakayewafaa kwa miradi tele ya maendeleo,” akasema Bw Moi.

Pia imebainika kwamba, Bw Moi analenga kuhakikisha kuwa anatokomeza umaarufu wa Naibu Rais katika eneo la Bonde la Ufa ili kupata nafasi bora ya kujadiliana na makabila mengine anakosaka uungwaji mkono.

Duru ndani ya kambi ya Bw Moi zilieleza Taifa Leo kwamba ameanza kujivumisha kwa kuwatumia waliokuwa wandani wa marehemu babake huku akilenga kutumia mikutano ya Jopokazi la maridhiano (BBI) kujisawiri kama mwanasiasa anayekubalika na mirengo yote ya kisiasa nchini.

Akilenga kuwavutia vijana kambini mwake, Bw Moi sasa amefufua kitengo cha vijana ndani ya Kanu huku akidai hilo litasaidia kupunguza umaarufu wa vuguvugu la Hasla linalohusishwa na Dkt Ruto.

“Ni kweli kwamba tumebuni kitengo cha vijana ambacho lengo lake ni kuvumisha BBI japo tunaelekeza macho yetu katika siasa za 2022,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Kanu George Wainaina.

Katika muda wa mwaka moja uliopita Bw Moi na wanasiasa wa Kanu wamezuru kaunti 15 katika kile kinachoonekana kama kurejeshea chama chake makali yake ya zamani.

Kati ya kaunti hizo ni Migori, Isiolo, Kajiado, Elgeyo-Marakwet, Pokot Magharibi na Lamu.

Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat alisema kuwa wanalenga kufufua chama hicho, akithibitisha kuwa macho yao yote yameelekezwa katika kiti cha Urais.

“Mara hii hakuna njia nyingine kwa sababu tunalenga kiti cha Urais kupitia nyapara wetu Gideon Moi. Tutaimarisha chama chetu kuanzia matawi nyanjani hadi kiwango cha kitaifa,” akasema Bw Salat.

Mbunge Mwakilishi wa kike wa Baringo Gladwell Cheruiyot kwamba wameona njia pekee ya kumwezesha Bw Moi kujiongezea umaarufu ni kuanzisha kampeni kali kote nchini badala ya kusubiri kuidhinishwa na Rais au kiongozi wa ODM Raila Odinga pamoja na nyapara wengine nchini.

“Hata kama ataidhinishwa, lazima pia aonyeshe ana wafuasi wengi. Wapinzani wetu huwa wanafurahia tukikimya lakini wanaona wivu na kutaabika wakiona umaarufu wetu unaongezeka,” alihoji Bi Cheruiyot.

You can share this post!

Kufanya refarenda bila sajili mpya ya wapigakura si haki...

Kesi ya mauaji ya Sharon kuanza rasmi, DPP asema