• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Kura ya maamuzi kufanyika Julai, asema Junet

Kura ya maamuzi kufanyika Julai, asema Junet

Na CHARLES WASONGA

MWENYEKITI mwenza wa sekritarieti ya BBI Junet Mohammed amedokeza kuwa kura ya maamuzi kuhusu Mswada wa BBI itafanyika Julai 2021.

Aliongea jijini Nairobi Jumapili Bw Mohamed ambaye pia ndiye Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa alisema mwezi wa kufanyika kwa mchakato huo umehamishwa kutoka Juni ili kufidia kucheleweshwa kwa ripoti ya kamati ya pamoja ya kamati za Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu mswada huo wa marekebisho ya Katiba, 2020.

Mbunge huyo wa Suna Mashariki alisema kuwa tofauti zilizoibuka miongoni mwa wanachama wa kamati hiyo, zitasuluhishwa kufikia Jumanne wiki hii.

“Kwa hivyo, tumekubaliana kwamba kura ya maamuzi inafaa kufanyika Julai 2021. Kamati hiyo ya pamoja itasuluhisha tofauti zake ndani ya siku mbili zijazo,” akawaambia wanahabari.

“Baada ya kamati hiyo kuwasilisha ripoti yake, tutauliza uongozi wa bunge ikiwa tutahitaji kufanya kikao maalum au tusubiri hadi Mei wakati ambapo Bunge la Kitaifa limeratibiwa kurejelea vikao vya kawaida,” akaeleza Bw Mohamed ambaye ni mwandani wa karibu wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Mswada huo wa marekebisho ya Katiba unatarajiwa kujadiliwa katika Seneti na Bunge la Kitaifa kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta autie sahihi.

Baada ya kuutia sahihi, Rais Kenyatta atawasilisha mswada huo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambayo itachukua muda wa mwezi mmoja kuandaa kura ya maamuzi.

You can share this post!

Barabara mbovu Githurai 44 kikwazo kwa wakazi kutembea

Hisia mseto miongoni mwa wadau wa soka kuhusu kipute kipya...