Hisia mseto miongoni mwa wadau wa soka kuhusu kipute kipya cha European Super League(ESL)

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL, Manchester City, Arsenal, Chelsea, Manchester United na Tottenham Hotspur ni miongoni mwa klabu 12 ambazo zimekubali kujiunga na kipute kipya cha European Super League (ESL).

Katika hatua inayotarajiwa kuathiri pakubwa kampeni za soka ya bara Ulaya, vikosi hivyo vikuu vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) vinaungana sasa na AC Milan, Atletico Madrid, Barcelona, Inter Milan, Juventus na Real Madrid.

Kwa mujibu wa vinara wa ESL, vikosi hivyo vimekubali kuanzisha kivumbi kipya kitakachokuwa kikinogeshwa katikati za wiki huku vikiendelea kuwa sehemu ya Ligi Kuu za mataifa yao mbalimbali.

Inatarajiwa kwamba kipute cha ESL kitaanza punde vikosi vitatu zaidi kutoka Ligi Kuu tano za soka ya bara Ulaya; yaani Ligue 1 (Ufaransa), Bundesliga (Ujerumani), La Liga (Uhispania), EPL (Uingereza) na Serie A (Italia) vitaunga mkono mpango huo.

Usimamizi wa ESL pia una mpango wa kuzindua kipute cha soka ya wanawake pindi baada ya kivumbi cha wanaume kuanza kutandazwa. Mbali na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, wengine ambao wamepinga hatua hiyo ya kuanzishwa kwa kampeni za ESL ni vinara wa EPL na Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa).

Kwa mujibu wa Uefa, kutekelezwa kwa mpango huo ambao msukumo wake umechochewa na tamaa ya fedha, kutavuruga na kuharibu ladha ya Ligi Kuu za mataifa mbalimbali na kushushwa viwango vya ubora vya vipute hivyo.

Kinyume na soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), washiriki wa ESL watasalia kuwa vikosi sawa 15 kila mwaka huku vitano vya ziada vikifuzu mwishoni mwa kila msimu.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limepinga hatua ya kuasisiwa kwa kipute cha ESL na kuonya kwamba wachezaji watakaonogesha mapambano hayo watanyimwa fursa ya kushiriki kampeni za Kombe la Dunia.

Kwa mujibu wa ESL, pambano hilo litakuwa na jumla ya washiriki 20 – wanachama 12 waasisi, klabu tatu za ziada zitakazojiunga na kipute hicho hivi karibuni na klabu tano zitakazokuwa zikifuzu kila mwaka kutegemea ubora wa matokeo yao kwenye Ligi Kuu za mataifa yao.

Kivumbi hicho kimependekezwa kuanza Agosti 2021 kwa mechi za katikati ya wiki ambazo zitashuhudia washiriki wakigawanywa kwenye makundi mawili ya klabu 10 zitakazokuwa zikicheza dhidi ya nyingine nyumbani na ugenini.

Washindi watatu wa kwanza kundini watafuzu kwa robo-fainali huku timu zitakazoambulia nafasi za nne na tano zikifuzu kwa mchujo wa mikondo miwili kuwania tiketi mbili za ziada.

Baada ya hapo, kipute hicho kitakumbatia mfumo wa UEFA wa kutandaza mechi za mikondo miwili za nusu-fainali kabla ya fainali itakayofanyika Mei katika uwanja usiokuwa wa nyumbani kwa washiriki wawili wa mwisho.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO